Chama la Wana ndivyo hivyo

Muktasari:

Kundi  moja lilikuwa likiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti Amani Vincent ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa klabu hiyo maarufu kama Chama la Wana na jingine lile lililobaki klabuni na lililofanya uchaguzi mkuu hivi karibuni.


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya Uchaguzi imekata mzizi wa fitina kwa kutamka wazi kuwa Stand United inamilikiwa na nani kati ya pande mbili zilizokuwa zikilumbana na kuleta mrafaruku mkubwa.

Mgogoro wa klabu hiyo ulikuwa ukihusisha wale wanaojiita Klabu na wale wa Kampuni, kila mmoja ikitangaza maamuzi yake ikiwamo suala la usajili wa wachezaji wa kikosi cha timu hiyo.

Mgogoro huo wa Stand United uliibuka mara baada ya kupatikana kwa mdhamini wao Kampuni ya uchimbaji Madini ya Acacia iliyowekeza Sh 2.4 bilioni kwa miaka miwili na tayari imemaliza mwaka mmoja.

Kundi  moja lilikuwa likiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti Amani Vincent ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa klabu hiyo maarufu kama Chama la Wana na jingine lile lililobaki klabuni na lililofanya uchaguzi mkuu hivi karibuni.

Tamko la TFF limesisitiza  kuwa wenye uhalali ni Stand United Klabu na kwamba wanachama waliofutiwa uanachama wataendelea kuwa halali akiwemo Amani na kwa hali hiyo ni kwamba klabu hiyo imezaliwa upya na muhimu haya yafanyike;


UMOJA

Stand United iliparaganyika na kukosa umoja, jambo lililopelekea kuwepo kwa mgogoro huo, hivi sasa viongozi walioingia madarakani kwa kuchaguliwa katika uchaguzi uliopitishwa na TFF wanapaswa kuunda umoja mpya kurudisha utulivu.

Bila umoja, hakuna jambo linaloweza kufanikiwa, umoja urudishwe kwa wanachama waliopo na wale waliorudishwa na TFF baada ya kutimuliwa na wanachama ambao waliona wenzao ni kama wasaliti, umoja huo unapaswa kuchagizwa zaidi na Amani.


USHIRIKIANO

Kurudishwa kwa wanachama waliofukuzwa waliofutiwa uanachama kunapaswa kuzika tofauti zilizoigawa Stand United. Hakuna haja ya watu kulauminiana maana dawa ya kufuta migogoro ilikuwa ni lazima uchaguzi ufanyike ili wapatikane viongozi halali na hili limeshafanyika.

Ikumbukwe tangu ipande Ligi Kuu, Stand haikuwa na viongozi wa kuchaguliwa zaidi ya wale wa kuteuliwa.

Ushirikiano wa waanzilishi wa klabu hiyo ambao walipambana kuhakikisha inapanda Ligi Kuu uheshimiwe na wale ambao wameikuta Stand tayari ipo kwenye sura ya kugombaniwa na kukubalika na kampuni kubwa kama Acacia.

Hivyo sasa ufunguliwe ukurasa mpya ili Chama la Wana lisonge mbele, hakuna kitu kinachoanzishwa bila chanzo hakika mgogoro huu ulikuwa na chanzo ambacho sasa mnatakiwa kukizika kabisa.


LIEWIG AWE HURU

Kila klabu inapofanya uchaguzi wake ni lazima kuwepo na Kamati ya Utendaji, lakini pia kuundwa kamati mbalimbali zenye nguvu ndani ya klabu. 

Jambo pekee ambalo wanapaswa kulitambua ni kumwacha kocha wao afanye kazi yake kama mtalaamu wa Benchi la Ufundi na sio kumwingilia kazi yake ikiwemo kupangiwa kikosi.

Kocha Patrick Liewig ni mtu mwenye misimamo mikali katika maisha yake ya soka, anachokiamini ndicho anachokifanya hivyo, ili asivurugwe  ni bora  asiingiliwe kwenye kazi yake vinginevyo mtaona ni kocha ambaye hafai na kuanza kumuundia zengwe, kila mtu afanye kazi kwa kufuata mipaka yake.


USAJILI

Baada ya ligi kumalizika, Liewig alikabidhi taarifa yake ya msimu mzima kwa viongozi na wadhamini ambao ndio mabosi wake, alipendekeza majina ya wachezaji ambao yeye anawaamini wanaweza kuisadia Stand ikiwemo gharama za usajili ambapo alitaka apewe Sh 80 milioni tu.

Kutokana na misimamo yake, Kamati ya Usajili isiongeze kitu cha nyongeza kwenye usajili kwa matakwa yao, kwani hawataumia wao, ila wachezaji. 

Hii ni kutokana na imani yake Mfaransa huyo ambaye hafichi kitu kwamba mchezaji ambaye hayumo kwenye mipango yake basi hata matumizi kwenye kikosi chake yanakuwa ni ya msimu.

Hiyo inaweza kupelekea mchezaji mwenyewe kushuka kiwango na baadaye hatafaa tena matokeo yake ni kujengeana chuki na majungu ndani ya timu. 

Usajili uzingatiwe matakwa ya kocha maana yeye ndiye anajua zaidi na mkumbuke kwamba Liewig hana staa anachoamini ndani ya timu yeye ndiye staa.


MDHAMINI

Kati ya klabu ambazo zimepokea barua nyingi za onyo kutoka kwa mdhamini wao Stand ni kinara, tangu mgogoro huu uanze Acacia imekuwa ikiwaonya viongozi wa klabu hiyo kuachana na migogoro ikitaka wakae meza moja wamalizane kwa amani. Kitu pekee walichokuwa wanapigania Acacia ni klabu hiyo kufanya uchaguzi ili wapatikane viongozi halali ambapo sasa watakuwa na amani na uwezekezaji wao kwani tayari uchaguzi ulifanyika.

Jambo lingine ambalo walipingana nalo kabisa ila hawakuweka mipaka juu ya mabadiliko ni juu ya Stand kuwa kampuni kwani katika mkataba wao wa makubalino ni kwamba wanaadhamini Klabu na si Kampuni, hivyo kidogo wajitoe klabuni.

Stand ni vema ikapigana kutunza udhamini huo kwani si kazi rahisi kumpata tena Acacia wakisepa zao.


DK. TIBOROHA

Amani alikuwa na wazo zuri la kufanya mabadiliko ingawa hakusoma alama za nyakati kuwa mabadiliko hayo yanafanyika kwa kipindi gani na ni akina nani anawafanyia mabadiliko hayo.

Amani alitaka kuendesha soka kisasa zaidi kwa haraka mno. 

Wazo lake halifi ipo siku atalifanyia kazi kwa muda uliopangwa.

Lakini bado kuna maswali kwa huyu Dk Jonas Tiboroha msomi wa PhD alivyoibukia Stand baada ya kuachana na klabu yake ya Yanga ambayo miaka kibao imeshindwa kugeuzwa kampuni.

Bila shaka kiongozi huyo anapaswa ajifikirie mara mbili na kama kweli alikuwa na nia ya dhati ya Chama la Wana aungane nao kuiendeleza klabu hata kama wazo la kampuni litaendelea kutafutiwa ufumbuzi taratibu.


TFF

TFF pengine ilikuwa inaogopa kivuli chake kutatua kwa haraka mgogoro wa Stand na tukisema TFF tunamaanisha kwamba Rais Jamal Malinzi, aliyeshindwa kutoa amri kama mzazi matokeo yake akaitumia Kamati ya Uchaguzi kumaliza mgogoro huo.

Bahati nzuri Kamati ya Uchaguzi chini ya Wakili Revocatus Kuuli asiye mwanasiasa aliweza kulimaliza tatizo, sasa ni vema ikawa makini katika hali kama iliyojitokeza Stand ili kuepuka kulivuruiga soka la Tanzania kwa sasa au kwa baadaye.

 Wawekezaji wanaweza kukatishwa tamaa pale wasimamizi wa soka wanapochelewa kuchukua maamuzi ya mapema kutuliza vurugu na migogoro kama iliyoibuka Chama la Wana.