Yanga ni kufa ama kupona kwa Medeama

Muktasari:

Katika mazingira hayo Yanga inapaswa kujipanga vizuri, huku ikibebwa na idadi kubwa ya mashabiki watakaoishangilia ili kushinda mchezo huo na kujipatia pointi tatu muhimu za kwanza.


WIKIENDI hii, wawakilishi pekee wa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki, Yanga itakuwa na kibarua kigumu katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati itakaposhuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuvaana na Medeama ya Ghana.

Hii ni mechi ya kufa au kupona kwa Yanga japo sio ya mwisho ya kuamua hatma yao ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo kupitia Kundi A, ambalo pia lina  timu za TP Mazembe ya DR Congo na MO Bejaia ya Algeria.

Ikumbukwe kuwa, katika mechi mbili za awali Yanga ilifungwa nyumbani na ugenini kila mechi bao 1-0, ilianza dhidi ya Bejaia kisha ikafuata Mazembe, hivyo kubakiwa na mechi nne mkononi mbili za nyumbani na mbili za ugenini.

Kwa namna yoyote ile Yanga inalazimika kushinda mchezo dhidi ya Waghana kwani, ushindi ndio utaweka hai matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Iwapo Modeama itapata ushindi katika mchezo huo, itafikisha pointi nne na kujenga ari mpya ya kuona kuwa inaweza kufanya vizuri jambo ambalo litakuwa baya kwa Yanga.

Waghana hao wakifanikiwa kushinda ugenini watajijengea mazingira ya kuamini kuwa, wana uwezo mkubwa wa kushinda mechi ya marudiano dhidi ya Yanga nyumbani kwao Ghana.

Katika mazingira hayo Yanga inapaswa kujipanga vizuri, huku ikibebwa na idadi kubwa ya mashabiki watakaoishangilia ili kushinda mchezo huo na kujipatia pointi tatu muhimu za kwanza.

Wapinzani wakubwa wa Yanga katika michuano hiyo ni Bejaia na Medeama ambazo zina pointi kati ya 1-4 na hali halisi inaonesha kuwa Mazembe ipo katika mazingira mazuri kuchukua nafasi ya kwanza kwani, imeshakusanya pointi sita mpaka sasa.

Jambo la kuomba ambalo litakuwa na manufaa kwa Yanga japo litakuwa linaijengea Mazembe nafasi nzuri zaidi na kuonesha ubora zaidi ni la kuiombea timu hiyo ya DR Congo kuzifunga Bejaia na Medeama katika mechi zake zote.

Ikifanya hivyo na Yanga ikafanikiwa kuzifunga pia timu hizo za Algeria na Ghana bila shaka yoyote itakuwa imeipa nafasi Yanga ya kuingia nusu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza. Iwapo matokeo yatakuwa hiyo Bejaia na Medeama hakuna timu itakayozidi pointi tano hivyo kuipa nafasi Mazembe na Yanga kuingia nusu fainali kutoka kundi A.

Hakuna muda mzuri na nafasi nzuri na kwenye kundi rahisi kama ambalo Yanga imelipata mwaka huu na ikifanya uzembe ikashindwa kuingia nusu fainali inaweza kuja kujuta kwa muda mrefu. Wakati wa kuandika historia mpya ndio huu.

Kwa jinsi timu kadhaa za Afrika zilivyokuwa ngumu haitarajiwi katika miaka ijayo kama Yanga au timu yoyote Tanzania itakayoingia katika hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika itapata kundi rahisi kama hili.

Kama Yanga itazifunga Medeama na Bejaia nyumbani na kutoka sare na Medeama ugenini nchini Ghana itafikisha pointi saba bila ya kuweka matokeo ya mechi yao dhidi ya Mazembe itakayochezwa mwishoni mwa mwezi ujao kufungia dimba.

Pointi hizo saba za Yanga zinatosha kuipeleka nusu fainali kutoka kundi A bila ya kujali matokeo ya mechi ya marudiano kati ya Bejaia na Medeama.

Kimahesabu mazingira ya Yanga kuingia nusu fainali ni makubwa kinachotakiwa kwa benchi la ufundi la timu hiyo na wachezaji kuweka pembeni na kuyasahau matokeo ya mechi mbili zilizopita. Yanga ijiandae kucheza na Waghana kama vile ndio inaanza mashindano hayo na nafasi yake ya kusonga mbele ipo katika nafasi ya mechi nne zilizobaki na mechi mbili zilizopita hazihusiki.

Wachezaji wa Yanga wanapaswa kujitoa na kujituma kwa nguvu zote katika michezo iliyobaki ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuingia nusu fainali. Pamoja na kwamba hata wakifungwa na timu hiyo ya Ghana bado ina nafasi ya kusonga mbele kimahesabu, lakini jambo hilo si zuri na kamwe wasiliruhusu hata kidogo.

Macho yote yapo kwa Yanga ni wajibu wao kutimiza wajibu kwa kuwafunga Waghana hao tena ikiwezekana bao za kutosha kwani, jambo hilo linawezekana na wala halina kikwazo chochote kutokana na kandanda safi linalochezwa na Yanga kwa sasa na hamasa kubwa ya mashabiki wake. 

Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar,Uhuru na Mzalendo,Bussiness Times[Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi.Alikuwa mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania[TEF].Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020