Kocha wa Mbeya City apata ufahamu Ligi Kuu

Muktasari:

Mbeya City ipo nafasi ya 11 msimamo wa ligi hiyo ,ikiwa imekusanya pointi 19 kwa mechi 18 ilizocheza ambapo ikifanikiwa kushinda mechi ya leo itakuwa imefikisha pointi 22 na kusogea katika nafasi za juu.

Mbeya. Kocha Mkuu wa Mbeya City, Ramadhan Nswanzurwimo amesema kwa sasa ameanza kuielewa ligi ya Tanzania Bara (VPL) kwani awali ilikuwa ikimpa wakati mgumu.

City ambayo leo inaikaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa,  ina kibarua cha kuhakikisha inavuna pointi tatu mbele ya wapiga debe hao kutokana na mchezo wao dhidi ya Njombe Mji kuambulia suluhu.

Kocha Nswanzurwimo alisema tangu achukue mikoba ya Kinnar Phiri alikuwa anajitahidi kuiga falsafa ya soka la Tanzania lakini mwisho wa siku timu yake ilikuwa ikiambulia kichapo na kujiweka katika nafasi mbaya zaidi kimsimamo.

‘’Hata zile mechi saba mfululizo tulizovuna pointi moja tu niliona kama ni wakati mgumu mno kwangu kutokana na kwamba nilikuwa najitahidi kuwapa wachezaji maelezo mazuri lakini wakiingia uwanjani tu wanafungwa,’’alisema

Aliongeza ‘Nilikuwa nabaki na maswali mengi kichwani mwangu kwamba hata Singida United na Lipuli ambao ni wageni kwenye ligi wanatushinda sisi ambao tunashiriki kwa mara ya tano kwenye ligi hii?, lakini kwa sasa ni mwendo wa mapambano’alisema Nswanzurwimo.

Alisema baada ya kukaa na benchi lake la ufundi pamoja na wachezaji wake waliweza kubaini kuwa kikosi kina mapungufu kadhaa likiwemo la kukosa umakini, lakini tangu mzunguko huu uanze anaona suala hilo limekwisha.

Alisema matarajio yake ni kuona timu hiyo inamaliza mzunguko huu wa pili vyema na kupata matokeo mazuri kwa mechi 12 zilizobaki hadi kufungwa kwa pazia hili la Ligi  kuu msimu huu.

City ipo nafasi ya 11 kimsimamo wa ligi hiyo, ikiwa imekusanya pointi 19 kwa mechi 18 ilizocheza ambapo ikifanikiwa kushinda mechi ya leo itakuwa imefikisha pointi 22 na kusogea katika nafasi za juu.