Riadha waiangukia JKT iwaruhusu wanamichezo wake Madola

ARUSHA. Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Riadha, Zacharia Barie inayotarajia kushiriki mashindano ya kimataifa ya jumuiya ya madola na mbio za dunia, ameiangukia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuomba kuwaruhusu wanaridha hao kushiriki mbio zilizoko mbele yao.
 Barie ambaye amepewa dhamana ya kuinoa kikosi cha timu ya Taifa ya wanariadha waliofikia viwango vya kushiriki mashindano ya mbio za kimataifa, amepata pigo baada ya wanariadha tisa kuondolewa na mwajiri wao JKT kambini yaliyoanza hivi karibuni mkoani Arusha kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi.
 Akizungumza mkoani Arusha, Barie amesema kuwa walikuwa na ndoto na kurudi na medali katika mbio zilizoko mbele yao ikiwemo mashindano ya mbio za dunia ya Machi 24 na Michezo ya Madola Aprili 4 hadi 15 hadi ndoto zao zimeanza kudumaa kutokana na kukosekana kwa wanariadha hao.
 “Mimi nadhani kuna kitu ndio maana jeshi wanatufanyia hivi lakini niwaombe uongozi wa JKT watusaidie katika kusogeza maslahi ya Taifa mbele kwa kutusaidia kuwaruhusu wanariadha hawa warudi kambini kujiandaa na mashindano yaliyoko mbele yao maana bila wao nadhani medali tutapata lakini kwa shida sana.”
 Alisema kuwa maandalizi waliyokuwa wameyafanya ni ya kurudi na zawadi lakini pia kuweza kuwashawishi wadau wakubwa wa michezo duniani kupata udhamini katika maandalizi na mashindano mbali mbali duniani hivyo kuwakatalia ni kuwanyong’onyeza.
“Nchi yetu kwa sasa iko katika ujamaa haina vita hivyo wafikirie mara mbili uamuzi wao huo na kuwaruhu waje kambini kwa ajili ya kupigania viwango vyao na medali zao lakini pia bahati yao kwenye makampuni makubwa ya udhamini.”