Simon Msuva ampa mzuka Habib Kyombo

Muktasari:

  • Pia, anaamini kama akijituma na kuzidi kujitambua, ipo siku watu wake wa karibu nao watava jezi yake.

STRAIKA Habib Kyombo, wa Mbao FC, amepewa mzuka wa kuzidi kufanya vizuri na staa wa Taifa Stars, Simon Msuva anayekipiga klabu ya Difaa El Jadida inayoshiriki Ligi Kuu, Morocco.

Kyombo alipewa zawadi ya jezi na Msuva ambayo anakiri kila anaipovaa, huwa inampa moyo na kuamini hata yeye ana uwezo wa kufika mbali. Pia, anaamini kama akijituma na kuzidi kujitambua, ipo siku watu wake wa karibu nao watava jezi yake.

“Ukiona mtu anavaa jezi yako na kufurahia jezi hiyo, inabidi utambue kuwa ina maana kubwa kwako. Hii jezi ya Msuva inanifanya nijitume vizuri ili kila mmoja atamani kuvaa jezi yangu huko mbeleni,” alisema na kusisitiza kuwa jina lake si Kiyombo bali ni Kyombo.

Kyombo aliongeza, amekuwa na kawaida ya kuzungumza mara kwa mara na Msuva, lakini lengo kuu huwa ni kupata ushauri na pia kumpa moyo wa kutokukata tamaa, huku akimsisitiza kuwa na moyo wa subira na nidhamu pia ya ndani na nje ya uwanja.