Simba yawatuliza Al Masry, mvua, umeme vyatibua

Muktasari:

Simba sasa inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya mabao 3-3 ili kusonga mbele katika mashindano hayo

Dar es Salaam. MASHABIKI wa Simba jana Jumatano walikuwa na furaha kubwa, baada ya chama lao kuupiga mpira mwingi na kuwakimbiza Al Masry na kuchomoa kipigo kwa Waarabu kabla ya gemu kusimama kwa dakika 12 kutokana na mvua kubwa iliyonyesha ghafla uwanjani hapo.

Simba yenye rekodi ya kuvutia nyumbani dhidi ya timu kutoka Afrika Kaskazini, ililazimisha sare ya mabao 2-2 kabla ya umeme kukatika uwanjani hapo kutokana na mvua kubwa iliyoanza kunyesha ghafla na kusimamisha pambano dakika ya 78.

Pambano hilo la kwanza la raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika lilipigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ambapo ilishuhudia nyota wa Simba, John Bocco na Emmanuel Okwi  wakirejea uwanjani na kuifungia timu yao mabao.

Nyota hao walikuwa majeruhi na kukosa baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara, kila mmoja alifunga bao kwa mkwaju wa penalti kila kipindi na kuzimia Al Masry iliyoshindwa kumuanzisha straika wao mkongwe, Aristide Bance.

Bocco aliipa utangulizi Simba bao la dakika ya 10 tu baada ya beki Mohammed Koffi kuunawa mpira langoni mwake na straika huyo kumchambua kipa wa Al Masry na kuamsha shangwe kwa mashabiki lukuki wa Simba waliofurika Taifa.

Hata hivyo bao hilo lilidumu sekunde chache tu kwani dakika moja baadaye Ahmed Gomaa aliisawazishia Al Masry bao kwa dakika moja tu baada ya mfungaji huyo kumalizia krosi iliyoshindwa kuokolewa na mabeki wa Simba.

Wamisri walipata bao la pili dakika ya 26 kupitia kwa Ahmed Shoukry kwa mkwaju wa penalti baada ya James Kotei kuunawa mpira na straika huyo kumchambua kipa Aishi Manula.

MFARANSA AGOMEWA

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Simba ikisaka bao la kusawazisha na Wamisri wakitaka kuongeza mabao na Kocha wa Simba, Pierre Lechantre alitaka kufanya mabadiliko ya kumtoa Shiza Kichuya, lakini wachezaji wake walimgomea huku wakiungwa mkono na mashabiki waliokuwa wakizomea mabadiliko hayo.

Kocha huyo aliamua kubadilisha mawazo ya kumtoa Kichuya na badala yake akamtoa Bocco ambaye hakuwa fiti na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo katika dakika ya 60, mabadiliko yaliyoisaidia Simba kuwa moto.

Dakika ya 73 Yusuf Mlipili alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla na kuifanya Simba izidi kuwaandamana Al Masry na dakika ya 74 shambulizi kali la Simba liliwachanganya mabeki wa Al Masry na kuunawa mpira na kuamuriwa adhabu ya penalti na Okwi kutumbukiza wavuni kuisawazishia timu yake.

Dakika nne baadaye mvua kubwa iliyonyesha ghafla ilisababisha umeme kukatika wakati Simba ikiwakimbiza Wamisri na kusimama kwa dakika 12 na mashabiki kuvamia uwanja na kujikuta wakichezea vichapo toka kwa askari polisi.

Baada ya majadiliano na hasa umeme ulivyorudi timu zilikubaliana kumalizia muda uliosalia, japo mchezo haukuvutia kutokana na uwanja kujaa maji na hivyo mpira kuchezwa kwa kubutuliwa juu kwa juu na timu zote zikikosa mabao ya wazi.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Katika mechi hii vilabu vyote vilikuwa vikicheza kandanda safi huku safu ya Simba ya kiungo ikionekana kuimarika baada ya kuwacheza viungo wawili wakabaji, Shomari Kapombe na Jonas Mkude huku wakimuacha Shiza Kichuya akifanya kazi yake.

Al Masry hawakuonyesha kucheza kwa kujilinda baada ya kufunguka mara kwa mara, huku wakilazima kupata mabo zaidi.

Licha ya kwamba ndio ilikuwa mara ya kwanza akiwa Simba msimu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, Kapombe alionyesha kuhimili nafasi hiyo vilivyo.

Kapombe aliongeza nguvu katika ukabaji akisaidiana na Jonas Mkude, hali ambayo iliwafanya Simba wacheze soka safi.

Kwa matokeo hayo Simba inalazimika kwenda kusaka ushindi wowote Port Said katika mchezo wa marudiano na mshindi kutinga hatua ya play-0ff kusaka za kutinga makundi.

Katika mechi nyingine za michuano hiyo ya Afrika Zamalek ikiwa ugenini ilifungwa mabao 2-1 na Welayta Dicha walioing'oa Zimamoto, Gor Mahia ililazimishwa suluhu nhyumbani na Esperance ya Tunisia na TP Mazembe ikashinda 4-0 nyumbani dhidi UD Songo ya Msumbiji.

 Zanaco walilala 2-1 nyumbani dhidi ya Mbabane Swallows sawa na ilivyokuwa kwa nduigu zao za Zesco United walichapwa 1-0 na ASEc Mimosas.

Simba: Manula, Kapombe, Kwasi, Mlipili/Ndemla, Nyoni, Mkude, Okwi, Kotei, Bocco/Mavugo, Gyan, Kichuya