Al Masry yaipa ubingwa Al Ahly

Muktasari:

Matokeo hayo ya Al Masry itakayocheza na Simba mwishoni mwa wiki hii katika mchezo wa marudiano umeifanya Al Ahly kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo huku wakiweka rekodi ya kunyakuwa taji hilo mara 40.

Cairo, Misri. Wapinzani wa Simba katika Kombe la Shirikisho Afrika, Al Masry wameikabidhi Al Ahly ubingwa wa Ligi Kuu Misri baada ya kukubali kulazimishwa suluhu na Entag El Harby jana Jumatatu usiku.

Matokeo hayo ya Al Masry itakayocheza na Simba mwishoni mwa wiki hii katika mchezo wa marudiano umeifanya Al Ahly kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo huku wakiweka rekodi ya kunyakuwa taji hilo mara 40.

Awali Al Ahly ilishinda bao 1-0 dhidi ya ENPPI shukrani kwa goli la Ayman Ashraf ikawa inasubiri matokeo ya mechi ya Al Masry ili kujihakikishia kutwaa ubingwa ikiwa na mechi sita mkononi.

Al Ahly hadi sasa haijapoteza katika Ligi Kuu ikiongoza kwa pointi 75 baada ya mechi 28. Ikifuatiwa na Ismaily (pointi 53), Zamalek (51) na Al Masry (49), hiyo inamaana kati ya timu hizo tatu hakuna itakayoifikia Al Ahly ataka kama itashinda mechi zake zote sita zilizobaki.

Hali hiyo itamfanya kocha wa Al Ahly,Hossam El-Badry kuwapa wachezaji wake wengi nafasi ya kucheza katika ligi, huku akiweka lengo lake la kunyakuwa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa ambalo wamelikosa tangu 2013.