VIDEO: Simba yaifuata Al Masry kibabe

Muktasari:

Simba inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya kimataifa baada ya kukosekana kwa miaka mitano

Djibouti City, Djibout. Vinara wa Ligi Kuu Bara. Simba baada ya kuiondoa Gendarmarie kwa ujumla ya mabao 5-0 sasa watacheza na Al Masry ya Misri katika raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mshambuliaji Emmanuel Okwi alifungia Simba bao pekee katika dakika 53 katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali kwenye Uwanja wa State de Vile jijini Djibouti.

Kwa ushindi huo sasa Simba itacheza na Al Masry ya Misri ambayo yenyewe imesonga kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-2 baada ya kufungwa 2-1 na Green Buffaloes ya Zambia.

Wamisri hao wakiwa na mshambuliaji wao kutoka Burkina Faso, Aristides Bance katika mchezo wa kwanza nyumbani Cairo iliwafunga Wazambia hao kwa mabao 4-0.

Ushindi huo mwembamba wa Simba ulitokana na mfumo wa Kocha Mfaransa Pierre Lechantre aliyeingia katika mchezo huo kwa kucheza kwa kujilinda na mfumo wake wa 5-4-1.

Mfaransa huyo baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 nyumbani aliamua kuanza mechi hiyo akiwa na mabeki watano Juuko Murshid, Nicholas Gyan, Asante Kwasi na Yusufu Mlipili pamoja na Erasto Nyoni katika safu yake ya ulinzi.

Huku akiwa akiwaweka benchi Shomari Kapombe na Said Ndemla hata hivyo kutokana na kuumia kwa nahodha John Bocco amelazimika kuanza na Emmanuel Okwi pekee katika safu ya ushambuliaji.

Okwi alisaidiana na Shiza Kichuya katika kupeleka mashambulizi wakati Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na James Kotei walitalawa katikati na kuwanyima kabisa nafasi Gendarmarie kucheza mpira.