Simba yaichapa Kagera Sugar yakaa kileleni

Muktasari:

Bocco ameweka rekodi ya kumfunga kipa Juma Kaseja mabao 10 tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu 2007

Kagera. Mabao ya Said Ndemla na John Bocco yametosha kuipa Simba ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Ushindi huo unaifanya Simba kurejea kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 32, wakifuatiwa na Azam (30) na Yanga (24) baada ya kila timu kucheza mechi 14.

Katika mchezo huo mshambuliaji Bocco ameendeleza rekodi yake nzuri dhidi ya kipa Kaseja kwa kufanikiwa kumfunga bao la 10 katika maisha yake ya soka.

Bocco amekuwa na rekodi ya kumfunga Kaseja kila wakati wanapokutana tangu mwaka 2007 alipoanza kucheza Ligi Kuu akiwa na Azam.

Bocco alisema “Kaseja ni kipa mzuri ndio maana anacheza mpaka leo katika kiwango chake na kumfunga magoli yote hayo kipa mahiri kama huyu si kitu raisi ila nashukuru Mungu nimeendelea kuwa na rekodi nzuri dhidi yake."
"Nitaendelea kupambana zaidi ya hapa ili kufunga zaidi ya magoli haya ambyo nimefunga ndani ya Simba ili kuisaidia timu yangu kufanya vizuri na kuchukua ubingwa msimu huu," alisema Bocco.
Naye Kaseja alisema mimi nipo katika nafasi ya kuzuia na Bocco yupo katika nafasi ya kufunga na ambaye atafanya vizuri zaidi ya mwenzake ndio atakuwa amefanya vizuri kama ilivyofanya mwenzangu katika mechi ya leo.

"Tunakwenda kujipanga katika mechi zijazo kwani matokeo kwa upande wetu si mazuri kabisa lakini naimani kocha ameona mapungufu kwenye mechi hii ambayo tulizamilia kushinda na atayarekebisha ili kufanya vizuri mechi ijayo," alisema Kaseja.
Mechi hiyo ilitawaliwa na ubabe wa hapa na pale na kusababisha hadi kufikia dakika ya 56, kadi za njano tano kutolewa na mwamuzi Shomari Lawi wa Kigoma.

 Wachezaji walionyeshwa kadi za njano ni Juma Nyosso, Mohammed Fakhi, Geroge Kavilla wote wa Kagera Sugar naJohn Bocco na Juuko Murshid wa Simba.

Nyosso alionekana kwenda bega kwa bega na Okwi katika mchezo huo lakini alipoonyeshwa kadi ya njano alionekana kupungua kasi ya kumkaba mganda huo.

Kagera wamiliki kiungo

Licha ya kwamba Kagera Sugar walipoteza mchezo huo walionekana kutakata eneo la katikati ya uwanja hasa kipindi cha pili lakini safu yao ya ushambuliaji ilikuwa  butu.

Nahodha George Kavila na Ally Nasorro walionekana kucheza vizuri eneno la kiungo hivyo kuwapa wakati mgumu viungo wa Simba, Jonas Mkude na Said Ndemla.

Safu ya ushambuliaji ya Kagera Sugar iliyoongozwa na Pastory Athanas, Japhary Kibaya na Atupele Green ilionekna akushindwa kabis akuipenya ngome ya Simba iliyoongozwa na Juuko Murshid na Erasto Nyoni.

Katika mchezo mwingine Majimaji imefanikiwa kuokota pointi mmoja muhimu baada ya kulazimisha sare 1-1 na Singida United.

Singida United ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Kambale Papy kabla ya wenyeji Majimaji kusawazisha katika dakika za mwishoni kupitia Peter Mapunda.