Nonga alimsha dude upya

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo alishindwa kutamba alipokuwa katika kikosi cha Yanga kabla ya kuomba kuondoka

Mshambuliaji wa Mwadui FC, Paul Nonga amesema bao alilowafunga dhidi ya Simba limempa mzuka wa kuendelea kupambana zaidi katika Ligi Kuu.

Nonga alifunga bao la kusawazisha katika mchezo uliopigwa Alhamisi iliyopta kwenye Uwanja Kambarage mjini Shinyanga wakati Mwadui ilipolazimisha sare 2-2 na Simba.

Bao hilo la dakika 89, liliwanyamazisha mashabiki wa Simba ni goli la tano kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga katika msimu wa Ligi Kuu.

Nonga alisema sasa kwake ndio ameanza Ligi kwani kila mechi amejipanga kufunga kwani bao hilo limempa nguvu kubwa ya kupambana.

“Hili bao limenipa nguvu ya kuendelea kupambana kwenye Ligi Kuu na sasa nitapambana kila mechi niweze kufunga na kuisaidia timu yangu,” alisema Nonga.

Mshambuliaji huyo alisema Ligi Kuu msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa wanahitaji kupambana vilivyo kama wanataka kuepukana na janga la kushuka daraja.