Simba walikufa mapema tu

Monday January 8 2018

 

By THOBAS SEBASTIAN, UNGUJA

MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi Azam FC, wameendelaa kuionea Simba baada ya kuifunga bao 1-0 juzi Jumamosi katika mechi kali na ya kusisimua.

Bao hilo murua lilifungwa na chipukizi Iddi Kipagwile aliyepokea pasi murua kutoka kwa Frank Domayo.

Ilikuwa ni kama marudio ya fainali ya mwaka jana ambapo Simba ilipokea pia kipigo cha bao 1-0. Lilikuwa ni bao la umbali mrefu la Himid Mao Mkami.

Katika mechi ya juzi, Azam haikuwa imara kama Simba, ingawa iliweza kutumia vizuri makosa ya wapinzani wao kupata matokeo ya ushindi. 

Kwa kifupi, Simba ilikufa mapema Uwanja wa Amaan kutokana na mambo kadhaa yaliyoigharimu kwenye mchezo huo ambao sasa umewaweka kwenye nafasi ngumu ya kufuzu nusu fainali. Simba italazimika kuifunga URA kwenye mechi ya mwisho inayopigwa jioni ya leo Jumatatu mjini hapa.

MFUMO MPYA

Simba ikiwa chini ya Mrundi, Masudi Djuma inatumia mfumo mpya wa 3-5-2 ambao bado haujaingia vizuri klabuni hapo. Licha ya kucheza vizuri, kuna makosa kadhaa ambayo yanaigharimu.

Mfumo mpya wa Simba umekuwa na makosa hasa katika safu ya ulinzi ambayo inakuwa na watu watatu tu. Mashambulizi ya kushtukiza ya Azam yalikuwa mwiba katika safu hiyo ya ulinzi.

Wachezaji wa Simba wanatakiwa kupata muda zaidi ili kuweza kutumia mfumo huo kwa ufasaha, kwani kwenye mechi ya Azam bado haukufanya kazi vizuri. 

UMAKINI MDOGO

Wachezaji wa Simba walikosa umakini hasa katika kushambulia kwani walitengeneza nafasi nyingi za kufunga hasa kipindi cha kwanza lakini walishindwa kuzitumia.

Dakika ya nane Simba ilikosa bao baada ya shuti kali lililopigwa na Mzamiru Yassin kutoka nje kidogo ya lango. Hali ilikuwa hiyo hiyo katika 14 alipokosa Said Ndemla, dakika ya 40 alipokosa John Bocco na mengine mengi.

Kama Simba ingeweza kuwa  makini na kutumia nafasi ambazo ilizitengeneza, basi ingeweza kumaliza mechi hiyo mapema. lakini hali haikuwa hivyo.

VIUNGO AZAM

Simba licha ya kujaza viungo wengi katika mechi hiyo, bado hawakuwa na ubunifu kama wale wa Azam. Simba ilianza na Jonas Mkude, Said Ndemla, Mzamiru Yassin na James Kotei huku Azam ikianza na Salmin Hoza na Stephane Kingue huku Himid Mao akicheza nafasi ya ulinzi.

Kingue na Hoza walicheza vizuri, wakijilinda kwa muda mwingi na kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza.

Baada ya kuingia Frank Domayo katika dakika ya 55 mambo yalikuwa magumu kwa Simba na ndipo bao lilipopatikana. 

ABALORA NOMA

Kipa wa Azam Razack Abalora alichaguliwa na jopo la makocha kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kweli alistahili kwani alifanya kazi yake kwa ufasaha kwa kuokoa hatari ambazo mashabiki wa Simba waliamini kwamba zingeweza kuazaa mabao.

 Abarola aliweza kuokoa michomo hatari ya Ndemla, Mzamiru, Bocco, na hata Jonas Mkude ambaye alipiga kichwa kikali katika dakika za lala salama na kuifanya timu yake kutoka kifua mbele.