Ubaya wa Simba ni mabao tu!

Muktasari:

Simba hawakufanya masihara katika kutupia mabao wakafunga 49 katika michezo 20, lakini   watani wao wa jadi Yanga, wao wamepachika mabao 38 waliyoyapa katika mechi 21 walizocheza  na kuweka tofauti ya mabao 11.

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga, wamepambana wee na sasa wamefikisha  pointi sawa na za Simba ambazo ni 46, lakini wao wanaendelea 'kusota'  chini kwa sababu wana idadi ndogo ya mabao huku Wekundu hao wa Msimbazi wakiendelea kutamba kileleni.
Simba hawakufanya masihara katika kutupia mabao wakafunga 49 katika michezo 20, lakini   watani wao wa jadi Yanga, wao wamepachika mabao 38 waliyoyapa katika mechi 21 walizocheza  na kuweka tofauti ya mabao 11.
Washambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda ndiyo kinara akiwa amefunga mabao 16, John Bocco 'Adebayor' yeye anashika nafasi ya pili kwao na tatu kwenye msimamo wa wafungaji bora wa ligi kuu na mabao 10, Shiza Kichuya ni wa tatu kwao na kwenye ligi kuu ni wa sita ana mabao saba wakati Mghana Asante Kwasi licha ya kucheza nafasi ya beki ni wa nne kwao na wa saba ligi kuu amefunga sita .
Kwa washambuliaji wa Yanga ni wawili tu ambao wana idadi kubwa ya mabao ambapo Mzambia Obrey Chirwa ndiyo kinara kwao wa mabao kwao na ni wa pili kwenye msimamo wa wafungaji bora ligi kuu akiwa na mabao 12, wakati Ibrahim Ajib anashika nafasi ya pili kwao na ligi kuu ni wa sita akiwa amefungana Kichuya wote wakiwa na mabao saba.
Hata hivyo, licha ya Simba kutamba kwenye ufungaji wa mabao katika kufungwa, wote wameruhusu mabao sawa langoni mwao ambayo ni 11 kwa kila mmoja.
Wafungaji wengine wanaotamba ligi kuu, anayeshika nafasi ya nne ni mchezaji wa Mbao Habibu Kiyombo aliyefungana na Eliud Ambokile wa Mbeya City wote wakiwa na mabao tisa, Mohamed Rashid wa Tanzania Prisons anashika nafasi ya tano akiwa amefunga manane.