Simba inatakiwa itulie, mihemko haitasaidia kitu

Muktasari:

Kwa mwaka Simba itakuwa ikipokea kiasi cha Sh888 milioni hii ikiwa maana kuwa, kila mwezi itavuna karibu Sh75milioni. Hizi sio kiasi kidogo cha fedha kwa klabu ambayo haina mdhamini wa aina yoyote.

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Klabu ya Simba ilifanikiwa kusaini mkataba wa miaka mitano na Kampuni ya Bahati Nasibu ya SportPesa wenye thamani ya Sh 4.96 bilioni.

Kwa mwaka Simba itakuwa ikipokea kiasi cha Sh888 milioni hii ikiwa maana kuwa, kila mwezi itavuna karibu Sh75milioni. Hizi sio kiasi kidogo cha fedha kwa klabu ambayo haina mdhamini wa aina yoyote.

Ni fedha nyingi kwa klabu ambayo inaishi kwa kutegemea hisani za mifuko ya watu wachache ambao mwishowe huwa si msaada bali ni deni linalopaswa kulipwa mara mwenye fedha zake atakapozitaka.

Inawezekana udhamini huo ukaonekana mdogo kwa ukubwa wa klabu ya Simba, lakini ni afadhali kuliko potelea mbali. Simba inapaswa kushukuru kwa kupata udhamini huo, hata kama umewakera baadhi ya watu ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakinufaika na hali ya maisha ya klabu hiyo.

Kwa namna Simba ilivyokuwa ikiishi ni afadhali ilivyoupata mkataba huo ambao kwa kiasi kikubwa utaipunguzia mizigo iliyokuwa nayo kuanzia kuhudumia timu na gharama nyingine klabuni kwao.

Bahati mbaya ni kwamba kuja kwa mkataba huo ni kama kumeleta sokomoko kutokana na vurugu zinazodaiwa kuanza kuinyemelea klabu hiyo ikiwamo baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji kujiengua.

Mbali na wajumbe kuanza kujiengua klabuni, pia aliyekuwa mfadhili wao Mohammed Dewji ‘Mo’ ametaka alipwe chake kwa kuchukizwa na kitendo cha viongozi wa Simba kumzunguka katika dili la SportPesa.

Pia, baadhi ya wanachama wa klabu hiyo hasa Baraza la Wadhamini nao wameibuka na yao wakidai hawajashirikishwa katika dili hilo, kiasi kwamba kama Wana Msimbazi hawatakuwa makini wanaweza kujiharibia mapema.

Wadhamini kama walivyo wafanyabiashara wengine hupenda mahala penye amani na utulivu ili kufanya shughuli zao pale wanapowekeza fedha zao, hivyo kama Simba haitakuwa makini inaweza kulipoteza dili waliloingia na SportPesa.

Ndio maana Mwanaspoti inawakumbusha wadau wa Simba wakiwamo viongozi, wanachama na hata mashabiki kuwa, ni lazima watulize akili zao kwa sasa.

Fedha zilizoletwa na mkataba walioingia na kampuni hiyo ya Kenya zisiwavuruge na badala yake wazidi kuwa na umoja na mshikamano kwa manufaa ya klabu yao.

Ni lazima wajifunze kutokana na hali ngumu iliyopitia klabu hiyo wakati mkataba wao na Kampuni ya Bia (TBL) ulipomalizika, kisha waone umujimu wa kutunza amani na utulivu ili kuwaacha wawekezaji walitua klabu kwao wawarahisishie kazi.

Kuendelea kuvurugana kwao sio tu kutawakimbiza wadhamini wao, lakini pia itaifanya timu yao ishindwe hata kumaliza vema Ligi Kuu Bara na ikikumbukwa kuwa mwishoni mwa mwezi watacheza fainali ya Kombe la FA mjini Dodoma.

Kama hawatakuwa na utulivu ni dhahiri wanaweza kupoteza mchezo wao dhidi ya Mbao FC na kujikuta wakikosa vyote kwa maana kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA na kushindwa kukata tiketi ya mechi za kimataifa mwakani.

Mara ya mwisho kwa Simba kuiwakilisha nchi ilikuwa mwaka 2013 iliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, je, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo wangependa kuendelea kutaniwa na watani zao kuwa ni Wazee wa Hapahapa?

Kama hawapendi utani huo, basi wapungumze mihemko, kwani kwa kipindi hiki haitawasaidia kwa lolote zaidi ya kuwavuruga.