Simba, Yanga hadi huku!

Muktasari:

Juzi Jumapili timu ya Simba Queens ilivaana na Evergreen inayopigilia jezi za rangi ya kijani, sawa na zile zinazovaliwa na Vijana wa Jangwani na kufanya kuungwa mkono na mashabiki wa upande huo hivyo kuwapa wakati mgumu wapinzani wao.

UTANI wa jadi haupo Simba na Yanga tu katika Ligi Kuu Bara, bali hata katika Ligi Kuu ya Wanawake nako kumekucha.

Juzi Jumapili timu ya Simba Queens ilivaana na Evergreen inayopigilia jezi za rangi ya kijani, sawa na zile zinazovaliwa na Vijana wa Jangwani na kufanya kuungwa mkono na mashabiki wa upande huo hivyo kuwapa wakati mgumu wapinzani wao.

Pambano hilo lilipigwa kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam na mashabiki wa pande hizo kulianzisha kwa kunogesha mchezo huo kwa kutambiana japo mwishowe Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ilikuwa hivi. Wafanyabiashara wa soko la Machinga Complex, waligawanyika makundi mawili, moja likiwa la Yanga walioishangilia Evergreen ambao huvaa jezi za kijani na wengine wa Simba waliokuwa wakiiunga mkono Simba Queens.

Mashabiki hao waliibua msisimko mkubwa na hasa baada ya Asha Rashid kuifungia Simba lao la mapema katika dakika ya nne tu.

Kocha wa Simba, Omary Mbweze alisema ushindi huo, utaibua nguvu mpya kwa mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao, akidai walikatishwa tamaa na matokeo ya mechi mbili za mwanzoni.

“Ni kama kwa timu ya wanaume, ikiboronga mashabiki wanaumia, lakini naamini kwa matokeo haya mambo safi,” alisema.