Simba, Singida United ni vita ya mapro 12 uwanjani

Dar es Salaam. Mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Simba na Singida United, umepambwa na ishara ya mabadiliko makubwa ya soka nchini.

Timu hizo zinatarajiwa kuteremka uwanjani leo huku zikinogeshwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni ‘mapro’ wanaotoka katika nchi tofauti Afrika.

Uwekezaji uliofanywa na klabu nyingi za Ligi Kuu ukiondoa Simba na Yanga, umechangia kuongezeka wachezaji wa kigeni hatua iliyoongeza ushindani wa namba.

Simba na Singida United zinatarajiwa kutumia takribani jumla ya wachezaji 12 wa kigeni wakati timu zao zitakapovaana kuwania pointi tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Kanuni za Ligi Kuu zinaruhusu klabu kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi saba, lakini huenda nyota 12 kutoka nje wakaanzishwa katika kikosi cha kwanza.

Kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima hatacheza mchezo huo, lakini wengine sita wana nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Simba ambao ni Asante Kwasi, James Kotei na Nicholas Gyan (Waghana), Juuko Murshid na Emmanuel Okwi (Waganda) na Laudit Mavugo (Mrundi).

Kwa upande wao Singida United itamkosa raia wa Rwanda, Dan Usengimana ambaye ni majeruhi lakini ina uhakika wa kuwatumia Michael Rusheshangoga (Mnyarwanda), Shaffiq Batambuze (Mganda), Malik Antiri (Mghana), Lubinda Mundia (Mzambia), Tafadzwa Kutinyu (Mzimbabwe) na Kambale Salita (Mnyarwanda).

Singida United imepata umaarufu tangu kuanza msimu huu baada ya kucheza kwa kiwango bora katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi mjini Unguja, Zanzibar.

Beki Batambuze ni mfano bora kwa timu hiyo baada ya kuchomoza mara tatu akipata tuzo ya Mchezaji Bora.

Vita ya ‘mapro’ inanogeshwa zaidi na uwepo wa makocha wa kigeni Mholanzi Hans Pluijm wa Singida United na Mrundi Masoud Djuma anayeinoa Simba.