Siku 1806 za mateso Msimbazi na yaliyojiri

Muktasari:

  • Yanga waliitaka sana Simba irudi, ili iwatie mzuka wa kufika mbali, kwani kushiriki bila mtani kwa miaka zaidi ya mitano kuliifanya ibweteke. Hakukuwa na wa kuwacheka.

WAMERUDI. Ndio, Simba imerudi katika michuano ya kimataifa. Nani ambaye hajatamani Simba irejee kwenye anga hizo? Kama wapo waliofurahia Simba kuwa nje ya michuano ya kimataifa basi ni wachache sana. Lakini ukweli hata wapinzani wao Yanga, licha ya kuwakebehi kwa kusota kwa siku 1806 bila kutia mguu katika anga hizo, kisirisiri waliokuwa wanaombea Simba irudi. Rekodi tamu ilizonazo Simba katika mashindano ya Afrika ni sababu ya kila mdau kuitaka irejee.

Yanga waliitaka sana Simba irudi, ili iwatie mzuka wa kufika mbali, kwani kushiriki bila mtani kwa miaka zaidi ya mitano kuliifanya ibweteke. Hakukuwa na wa kuwacheka.

Simba ina rekodi tamu katika mashindano hayo ya kimataifa na tamu zaidi ni ile ya kufika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 ambayo haijawahi kufikiwa na timu yoyote nchini, ikiwemo Yanga.

Simba pia ndio timu pekee ya Tanzania iliyofika Nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (enzi za Klabu Bingwa Afrika) mwaka 1974 kabla ya Malindi ya Zanzibar kufanya hivyo kwenye Kombe la CAF mwaka 1994.

Simba pia ndio walioweza kuwatoa waliokuwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek ya Misri mwaka 2003, wakitetemeshwa na Simba ya kina Juma Kaseja, Seleman Matola, Boniface Pawasa na Christiopher Alex.

Kama hujui, zimepita siku 1806 tangu Simba ilipocheza mechi yake ya mwisho ya kimataifa. Ukihesabu haraka haraka ni sawa na saa 43,344. Ni muda mrefu sana kwa timu ya soka kongwe na maarufu kuwa nje ya mashindano ya CAF.

Ilicheza mchezo huo wa mwisho Machi 3, 2013 na Recreative De Libolo nchini Angola na kulala 4-0, yaani 4G. Wiki mbili nyuma ilikubali kipigo cha bao 1-0 jijini Dar es Salaam kutoka kwa Waangola hao kabla ya kwenda kufa kinyonge Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Calulo. Tangu hapo Simba imekuwa ikiyasikia tu mashindano ya Afrika.

Kama ni mtoto amezaliwa, akaketi, akatambaa, akatembea, akakimbia na sasa yupo shule na anapiga kizungu freshi kabisa lakini Simba haijacheza mechi nyingine ya kimataifa.

Hatimaye Mnyama amerudi kwenye mashindano hayo na leo Jumapili jioni atakinukisha Uwanja wa Taifa dhidi ya Maafande wa Gendamarie ya Djibouti. Ni mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika na timu itakayofuzu hatua ya makundi tu, itakuwa imejihakikishia Dola 150,000 (Sh336 milioni).

Makala haya yanaangazia kwa kina baadhi ya vitu vikubwa vilivyotokea kwenye medani ya soka nchini kipindi cha siku 1806 za mateso kwa Vijana wa Msimbazi.

YANGA YAFANYA KWELI

Simba imekuwa ikiibeza Yanga, eti inatisha kwenye soka la nyumbani lakini ikifika katika mashindano ya kimataifa inakuwa hoi. Hata hivyo wakati Simba ikiwa ‘eda’, Yanga ilifanya kweli na mwaka 2016 ikafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Hiyo ilikuwa rekodi nyingine kwa Yanga, kwani imekuwa klabu pekee ya Tanzania kufanya hivyo na ikumbukee mwaka 1998 ilikuwa pia ya kwanza kwa klabu za Tanzania kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa kabla ya Simba kujibu 2003.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, walifuzu hatua hiyo baada ya kuiondosha GD Sagrada Esparanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1.

Bahati mbaya kwa Yanga ni kama ilivyokuwa mwaka 1998 haikutamba katika mechi hizo za makundi kwani iligeuka kibonde na kuchapwa na timu zote, hivyo kumaliza mkiani na pointi nne tu.

SAMATTA REKODI KIBAO

Wakati Simba ikiendelea kukimbizana na Ndanda na Majimaji kwenye soka la ndani, staa wa Tanzania, Mbwana Samatta aliweka rekodi za maana hapa nchini, huko Jamhuri ya Kongo na Afrika nzima.

Kwanza, Samatta pamoja na Thomas Ulimwengu waliweka rekodi ya kuwa nyota wa kwanza wa Tanzania kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na walifanya hivyo mwaka 2015 wakiwa na TP Mazembe.

Akaongeza rekodi nyingine baada ya kuwa mfungaji bora wa Ligi hiyo ya Mabingwa sambamba na Bakri Al-Madina wa Sudan, kila mmoja akifunga mabao saba.

Staa huyo akaweka rekodi nyingine Januari 2016 baada ya kutangazwa Mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza Ligi za Ndani na wiki chache baadaye akajiunga na KRC Genk ya Ubelgiji.

RAGE HADI AVEVA

Simba ilianza kukosa mashindano ya kimataifa wakati ikiwa chini ya Mwenyekiti wa Aden Ismail Rage, yaani cheo cha urais ndani ya klabu hiyo kikiwa bado hakijazinduliwa. Rage aliondoka madarakani Juni 2014 baada ya kumaliza muhula wake wa kwanza na kugoma kugombea tena. Rage ndiye aliyeisaidia Simba kubeba taji la Ligi Kuu Bara 2012 na kushiriki michuano ya mwisho ya CAF 2013.

Baada ya Rage ukaja uongozi mpya chini ya Rais, Evans Aveva ambaye kama kusingekuwa na mchakato wa mabadiliko, Juni mwaka huu angekuwa anamaliza muhula wake wa kwanza.

Yaani Aveva katika miaka yake minne amefanikiwa kuibeba timu hiyo ishiriki mashindano ya kimataifa mara moja tu. Inashangaza sana.

Habari mbaya zaidi ni kwamba Simba hadi inarejea kwenye mashindano hayo, Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wako rumande wakikabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha.

Simba pia ilianza mchakato wa mabadiliko na tayari imemtangaza bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ kama mshindi wa zabuni ya kuwa mwekezaji mkubwa kwa dau la Sh20 bilioni akichukua asilimia 50 ya hisa japokuwa serikali imesisitiza anaruhusiwa kumiliki 49% tu.

MATAJI MATANO AZAM

Wakati Simba ikisaka tiketi ya kimataifa, Azam FC imefanikiwa kuzichanga karata zake na kushinda mataji matano tofauti.

Mwaka 2014 ambao ndio ulikuwa wa kwanza kwa Simba kukosa mashindano ya kimataifa, Azam ilianza kampeni yake ya kusaka mataji vizuri baada ya kusepa na ubingwa wa Ligi Kuu Bara tena kwa rekodi ya aina yake ya kucheza msimu mzima bila kupoteza mchezo hata mmoja.

Azam ikatwaa tena taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mwaka 2015 tena kwa rekodi ya aina yake ya kutopoteza mchezo wowote wala kuruhusu bao.Mwaka 2016 ikabeba taji la Mapinduzi kwa rekodi ya kutoruhusu bao lolote kabla ya kutwaa tena ubingwa wa Ngao ya Hisani miezi minane baadaye.

Mwaka huu Azam wamekamilisha taji la tano baada ya kusepa na lile la Mapinduzi kwa mara nyingine tena.

MBEYA CITY YAJA, YAPOTEA

Simba ikiwa kwenye eda ya muda mrefu, klabu mpya ya Mbeya City ilipanda Ligi Kuu Bara na kufanya makubwa kabla ya baadaye kushuka kiwango na kuwa timu ya kawaida.

Mbeya City ilitikisa mwaka 2013/14 na mbali na kuzipa changamoto timu kubwa, ilimaliza msimu ikiwa katika nafasi ya tatu. Ilikuwa nafasi ya juu zaidi kuwahi kushikwa na timu hiyo katika historia yake.

Msimu uliofuata ilivuta mkwanja wa maana baada ya kupata udhamini kutoka kampuni ya Binslum kupitia bidhaa yake ya RB Battery. Ilipata pia udhamini wa Coca Cola na mambo mengine ya maana. Wakati huu Simba inarejea kwenye michuano hiyo, Mbeya City imeshakengeuka na kuwa ya kawaida.

MSUVA TUZO TATU, ASEPE

Simba buana, kweli ilikuwa hoi. Muda ambao imekosa mashindano ya kimataifa, ulimtosha staa wa Tanzania, Simon Msuva kufanya yake na kusepa.

Katika kipindi hicho, Msuva alifanya yake akiwa na Yanga kisha kutimkia nchini Morocco alikojiunga na klabu ya Diffaa EL Jadida.

Msuva ambaye anatajwa kuwa winga mwenye kasi zaidi nchini, alitwaa tuzo tatu tofauti katika kipindi hicho ambacho Simba ilikuwa ‘matopeni’.

Nyota huyo wa zamani wa Moro United alikuwa mfungaji bora Ligi Kuu mwaka 2015 na 2017, huku pia akitangazwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu mwaka 2015.

MALINZI AINGIA NA KUTOKA TFF

Kitu kingine kikubwa ambacho kimetokea wakati Simba ikiwa nje ya mashindano ya kimataifa ni Jamal Malinzi.

Malinzi alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Oktoba 2013, ikiwa ni miezi sita tangu Simba ilipocheza mechi yake ya mwisho ya kimataifa.

Katibu huyo wa zamani wa Yanga, akaingia TFF, akalivuruga soka la Tanzania kwa kadri alivyoona inafaa. Akaivuruga Taifa Stars pamoja na kufanya mambo mengine ya msingi kama kuanzisha tena Kombe la FA, Ligi ya Vijana na Wanawake.

Simba ikiwa bado haijacheza mechi nyingine ya kimataifa, Malinzi alimaliza muhula wake wa kwanza na kwa bahati mbaya akashindwa kugombea kwa mara nyingine kutokana na kushtakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha na kughushi nyaraka.

Hata hivyo, bahati nzuri ni kwamba michuano ya FA ndiyo iliyoipa Simba tiketi ya mechi za kimataifa baada ya kuifunga Mbao FC ya Mwanza kwa mabao 2-1 ndani ya muda wa nyongeza na Malinzi ndiye aliyewakabidhi taji lao kabla ya majanja kumkuta.

BABU SEYA AACHIWA

Hili sio la soka lakini limetokea wakati Simba ikihaha kurejea kimataifa. Kama ulikuwa hufahamu, Simba ilishiriki mashindano ya mwisho wakati Babu Seya pamoja na mwanaye, Papii Kocha, wakiwa gerezani kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha, lakini wakati huu wanarejea kwenye mashindano hayo, wawili hao wako mtaani wanapeta.

OKWI NA RUTI ZAKE

Leo mashabiki wa Simba wanatembea kifua mbele kisa makali ya Emmanuel Okwi, lakini Mganda huyo mara baada ya kuipa timu hiyo taji la Ligi Kuu na kushiriki nao mara ya mwisho kwenye michuano ya CAF alitimka zake.

Aliuzwa Etoile du Sahel ya Tunisia kabla ya kurudi kwao kuichezea SC Villa kisha kujiunga na Yanga, lakini Simba ikiendelea kusotea tiketi ya mechi za kimataifa.

Simba walimchukua mwaka 2014 na kuichezea kabla ya kutimkia zake tena kwenda Denmark alipokwenda kuchemsha na kuamua kurejea kwao Uganda, huku Simba ikihaha kusaka tiketi ya michuano ya CAF.

Hata hivyo, kwa sasa mchezaji huyo amerejea tena kwa mara ya tatu huku timu yake ikiwa tayari imeshanasa tiketi ya kimataifa na leo ataliamsha dude na wenzake.