Sauti za Busara wamkuna Mzungu Kichaa

Saturday February 10 2018

 

By Rhobi Chacha

Zanzibar. Mwanamuziki mwenye asili ya Denmark, Mzungu Kichaa amesema mwaka huu Tamasha la Sauti Za Busara limezidi kuwa zuri na kwa upande wa sauti imekuwa bora zaidi.

Mzungu Kichaa alisema ameifurahia ‘Sound’ ya mwaka huu kwani imekuwa ya kimataifa tofauti na miaka ya nyuma hali  ilikuwa ni ya kawaida.

“Hii ni mara ya pili kushiriki Tamasha la Sauti za Busara ni nilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2010, hivyo miaka nane imepita.”

Mbali ya Mzungu Kichaa wanamuziki wengine wa kundi la Matonas'  Culturual group, Mwanahawa Ally na Patricia Hillary wamesifia mafanikio ya tamasha hilo.

 Mwanahawa alisema unajua mimi ni mara yangu ya pili kushiriki katika Tamasha hili la Sauti Za busara, la kwanza lilikuwa ni muda mrefu sana, ila sahizi naona kuna utofauti mkubwa sana, yaani katika tamasha hili wenyeji wachache ila wageni ni wengi tofauti na kipindi nilichowahi kuja kutumbuiza miaka mingi iliyopita.

"Sijajua kama muda ni bado au kwa wenzetu wa nje ya nchi ndio wamepata kulielewa zaidi tamasha hili, ila inapendeza sana na nimefurahi kuona wazungu wanacheza muziki wetu wa taarabu asilia," alisema Bi Mwanahawa.

Naye Patricia alisema hata mimi ni mara yangu ya pili kuja kutumbuiza katika Tamasha hili la Sauti za Busara, yaani nimefarijika sana kuona mashabiki damu zao hazijalala, si unajua mimi nikiwa jukwaani huwa napenda sana kucheza.

“Mashabiki walivyokuwa wakicheza  wananipandisha mzuka kweli tamasha hili wamejiandaa vizuri sana na sijaona mapungufu yeyote zaidi ya kufurahia wazungu wakicheza taarabu inapendeza ,"alisema Hillary.