Sanchez apiga selfie ndani ya Old Trafford

Muktasari:

Sanchez anatazamiwa kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika historia ya Ligi Kuu England

London, England. Mshambuliaji Alexis Sanchez amejipiga picha akiwa amevaa jezi ya Manchester United kwa mara ya kwanza katika kuthibisha uhamisho wake wa kwenda Old Trafford.

Mshambuliaji huyo wa Chile aliwasili kwenye Uwanja wa mazoezi wa Carrington katika kukamilisha uhamisho wake akitokea Arsenal.

Picha ya mshambuliaji huyo mwenye miaka 29, akiwa amesimama ndani ya uwanja wa Old Trafford na kujipiga picha ‘selfie’ akiwa amevalia jezi ya Manchester United

Sanchez anataraja kutangazwa rasmi leo, Jumatatu kuwa mchezaji wa Man United baada ya kuafikiana katika mahitaji yake binafsi.

Uhamisho wa Sanchez kwenda Manchester United umekamilika baada ya Henrikh Mkhitaryan kukubali kwenda Arsenal.

Jana Jumapili ilithibitishwa kwamba mastaa hao walikuwa wamekwenda katika pande tofauti kwa uhamisho wa kubadilishana bila hata ya senti ya pesa kuhusika na kila mmoja alikuwa katika mji mwingine kwa ajili ya vipimo vya afya.

Mkhitaryan staa wa kimataifa wa Armenia amekubali kutua Arsenal na hiyo jana alionekana katika hoteli moja jijini London akiwa na wakala wake, Mino Raiola, kwa ajili ya kuchukuliwa vipimo vya afya katika uwanja wa mazoezi wa Arsenal.

Awali staa huyo alikuwa ameachwa katika kikosi cha Manchester United ambacho kilishinda bao 1-0 ugenini katika pambano la Ligi Kuu England juzi Jumamosi mchana na Sanchez pia alikuwa ameachwa katika kikosi cha Arsenal ambacho kilishinda mabao 4-1 dhidi ya Crystal Palace, pale Emirates.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, hakuficha ukweli kwamba alimuacha Sanchez nyumbani kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake wa kwenda Manchester United huku pia akikiri kwamba dili hilo lilikuwa la kubadilishana na Mkhitaryan.

“Sikumchukua kwa sababu kulikuwa na suala la yeye kwenda Manchester United. Hauwezi kuwa na mawazo mawili halafu bado ukacheza mpira,” alisema Wenger.

Baadaye Sanchez alionekana jijini Manchester akisubiri vipimo vya afya kwa vile madaktari wa timu hiyo walikuwa wamesafiri kwenda Burnley katika mechi ya Ligi Kuu.

Alitazamiwa kufanyiwa vipimo hivyo juzi usiku baada ya timu hiyo kurejea.

Kocha wa United, Jose Mourinho, alikuwa amethibitisha bosi wake mtendaji, Ed Woodward na Makamu Mwenyekiti, Matt Judge, pamoja na bosi wa masuala ya fedha walikuwa wanafanya juu chini kuhakikisha Sanchez anatua kwa ajili ya kuongeza staa mwingine katika nafasi ya ushambuliaji.

Winga wa kimataifa wa Ufaransa, Anthony Martial alifunga bao pekee la ushindi katika mechi hiyo na Mourinho anaamini kwamba kikosi chake kinahitaji mchezaji mwingine wa mbele kwa ajili ya kuongeza machaguo yake.

“Kwa sasa hakuna ushindani wa nafasi, tuna washambuliaji wanne halafu tuna nafasi tatu. Ni mchezaji mmoja tu ndiye anakaa benchi. Ukiangalia nafasi ya ushambuliaji tunahitaji ushindani wa ndani zaidi,” aliongeza Mourinho.

Sanchez ambaye ni staa wa kimataifa wa Chile, anatazamiwa kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika historia ya Ligi Kuu England huku United ikitazamia kumpa kati ya Pauni 400, 000 hadi 500, 000 kwa wiki kabla ya makato ya kodi.

Madai makubwa ya mshahara ya Sanchez inasemekana ndio chanzo cha Manchester City na Chelsea kuachana na mpango wa kumchukua staa huyo, lakini Mourinho alikuwa amepania kuona Sanchez anatua Old Trafford katika dirisha hili.

United imempa mkataba wa miaka minne na nusu Sanchez mwenye umri wa miaka 29 huku akithaminishwa kwa dau la Pauni 35 milioni katika dirisha hili ingawa angeweza kuondoka bure Arsenal mwishoni mwa msimu huu.

Wakala wa staa huyo amelipwa kiasi cha Pauni 10 milioni na United huku nyota huyo mwenyewe akipewa kiasi cha Pauni 20 milioni kama kifuta jasho chake cha kukubali kusaini Manchester United katika dirisha hili na kuachana na mpango wake wa kwenda Manchester City.