Jezi ya Sanchez yaanza kuuzwa mitaani

Muktasari:

Mshambuliaji huyo wa Chile amekuwa na mafanikio tangu alipotua Arsenal akitokea Barcelona na sasa anakwenda Man United

London, England. Uhamisho wa Alexis Sanchez kwenda Manchester United umeiva baada ya Adidas kuchapisha jezi yenye namba 7 ya nyota huyo na kuanza kuizuza katika maduka yake ya mitaa ya Oxford, London.
Mshambuliaji huyo Sanchez atakuwa akipokea mshahara wa pauni 450,000 kwa wiki, tangu jana Ijumaa jezi zake zimeanza kuuzwa madukani.
Mshambuliaji huyo wa Chile amepewa jezi namba 7, iliyovaliwa na wachezaji nyota kadhaa waliopita Man United kuanzia George Best, Eric Cantona, David Beckham na Cristiano Ronaldo.
Katika duka la Adidas lililopo London's Oxford Street, shabiki wa kwanza wa Man United kununua jezi ya Sanchez alikuwa ni Amer Mourad.
Sanchez atakuwa akipokea mshahara wa pauni 350,000 kwa wiki, pamoja na pauni 100,000 za haki za matangazo kila wiki hivyo kuingiza pauni 7.5milioni kwa mwaka katika miaka yake nne ya mkataba aliyosaini.
Kocha Arsene Wenger amesema Sanchez kuondoka Arsenal haiwezi kuuma sana kama kipindi kile cha Robin van Persie alipoondoka kwenda Manchester United mwaka 2012.
Tukio hili la Sanchez linafananishwa na lile la Van Persie alipoondoka Arsenal na kwenda kujiunga na Man United moja kwa moja, ambako katika msimu wake wa kwanza tu akabeba taji la Ligi Kuu England.
Lakini, Wenger anachoamini kwamba mashabiki wa Arsenal watakuwa wamechoshwa na mambo ya Sanchez, hivyo kuondoka kwake hakuwezi kuwa na maumivu kama yale yaliyosababishwa na Van Persie alipotua Old Trafford kwa uhamisho wa Pauni 24 milioni miaka sita iliyopita.
“Tulimchukua Van Persie kipindi hicho alipokuwa akicheza mechi za rizevu Feyenoord," alisema Wenger juzi Alhamisi.
"Tulifanya kazi kubwa sana na alipokuwa kwenye kiwango bora akahama na hakika iliuma kwelikweli.”
Henrikh Mkhitaryan wa Man United anatarajia kuwa sehemu ya dili hilo yeye akitumkia Arsenal kuchukua mikoba ya Sanchez na Wenger anasema: “Mashabiki wetu wanafahamu wazi kwamba Alexis hatasaini mkataba mpya, wamekubaliana na hilo, hivyo kila kitu kinafahamika bayana.
“Hata hivyo, si tu ataondoka bali kuna faida nyingine inapatikana. Haiwezi kuumiza sana. Tunapoteza mchezaji sawa, lakini tunapata mchezaji mwingine. Anadhani ni jambo moja tu, kila mtu anakwenda kumrithi mwenzake huko anakokwenda.”