Safi sana Serengeti Boys, Felix ila msibweteke

Muktasari:

  • Serengeti imefuzu raundi ya tatu ya michuano hiyo kusaka tiketi ya fainali hizo zitakazofanyika nchini Madagascar kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na sasa itavaana na Congo ambayo iliiondosha Namibia.

JUZI Jumapili Watanzania walikuwa kwenye furaha kubwa, timu yao ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys ilipata ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Amajimbo ya Afrika Kusini katika mbio za kuwania Fainali za Afrika za mwakani.

Serengeti imefuzu raundi ya tatu ya michuano hiyo kusaka tiketi ya fainali hizo zitakazofanyika nchini Madagascar kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na sasa itavaana na Congo ambayo iliiondosha Namibia.

Aidha kwenye michuano ya Olimpiki iliyomalizika pia juzi Jumapili, mwanariadha Alphonce Felix, alionyesha ushupavu kwa kumaliza mbio za kilomita 42 (marathoni) katika nafasi ya tano.

Felix alitumia muda wa Saa 2:11:15 ikiwa ni tofauti na dakika 2:31 alizotumia mshindi wa mbio hizo, Eliud Kipchoge aliyekimbia kwa Saa 2:08:44.

Ni kweli Felix hakufanikiwa kupata medali kwenye mbio hizo, lakini nafasi aliyomaliza ni ya kupongezwa kwani alionekana alikuwa na kiu ya kuibeba Tanzania kwenye Olimpiki baada ya wenzake Said Makuka na Fabiano Joseph kukwama.

Makuka alimaliza katika nafasi ya 43 wakati Fabiano alikamata nafasi ya 112 kati ya wakimbiaji 155.

Hakuna ubishi timu ya Tanzania kwenye michuano ua Olimpiki iliyokuwa ikifanyika imetoka kapa kwa kushindwa kwa mara nyingine kuambulia hata medali, moja lakini bado tunapaswa kumtia moyo Felix ili kutokata tamaa wala kubweteka ili aje kuitoa kimasomaso Tanzania miaka ijayo.

Mwanariadha huyo anatakiwa kuanza kujiandaa na michuano ya olimpiki inayokuja kuanzisa sasa.

Ikumbukwe kwa jitihada za dhati na za muda mrefu ndio msingi wa maendeleo kwa mchezaji au timu fulani.

Wanariadha walioshika nafasi ya kwanza ya pili na ya tatu ni watu kama watu wengine kwa hiyo hakuna kitakachoshindikana kama mtu akijituma kwani watu hao hawatokei sayari ingine.

Wito kama huo pia tunautoa kwa vijana wa Serengeti Boys ambao wamebakisha hatua moja kuweka rekodi kama ya mwaka 2004 Tanzania ilipofuzu fainali kama hizo za U17 kabla ya kubainika kufanyika udanganyifu na timu kuondolewa.

Kuna kila sababu ya kujivunia vijana hawa walio chini ya jopo la makocha wanaoongozwa na Bakar Shime, kwani kazi waliyofanya mpaka sasa ni kubwa, lakini hatupaswi kuridhika ni lazima Serengeti Boys waing’oe Kongo ndipo wasonge mbele. Ikumbukwe kwamba ushujaa katika michezo unapatikana kwa kushinda uwanjani na si vinginevyo.

Hatutaki ile hadithi ya mtu kula ng’ombe mzima kisha kushindwa mkia ijirudie kwa vijana wetu, tuwatie moyo, tuwahamasishe na kuwaunga mkono kwa hali na mali mpaka pambano lao la mwisho la hatua ya mtoani ili waende Madagascar kwa ajili ya kuwakilisha taifa letu.

Kwa kuwa umri wao ni mdogo, kuna uwezekano mkubwa wa kuonekana kimataifa na huo ni mwanya kwao wa kununuliwa kama wakifanya vizuri.

Lakini kununuliwa kwa wachezaji kunatokana na suala zima la timu kufika mbali. Hakuna klabu ambayo inaweza kununua wachezaji ambao hawajafikia kiwango kizuri.

Kama tutaridhika mapema yanaweza kutukuta yaliyowahi kuikuta Taifa Stars mwaka 2007 wakati ikisaka tiketi za fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2008 zilizofanyika Ghana kwa kukwamishwa mwishoni na Angola.

Ndio maana Mwanaspoti linawapongeza Serengeti Boys na Alphonce Felix kwa walichokifanya juzi, lakini tukiwakumbusha kuwa bado wana safari ndefu hivyo wasibwete na kuona wameshamaliza kazi.