Ruvu Shooting yawapamba mashabiki

Muktasari:

Uuzaji wa jezi imekuwa ni moja ya chanzo cha mapato kwa timu nyingi duniani

Kisarawe. Ruvu Shooting ya Masau Bwire, kumbe  wajanja kinoma. Mabosi wao walikaa chini na kuangalia namna amshaamsha ya mashabiki wanaoiunga mkono na fasta wakapata akili ya kuwatengenezea jezi zilizozinduliwa jioni ya leo.

Jezi hizo zimezinduliwa na kuuzwa kwa mashabiki wao kwa Sh20,000 lengo likiwa ni kuichangia timu yao.

Kaimu Mwenyekiti wa Ruvu, Meja Michael James, alisema wamekuwa wakisaidiwa kwa namna moja ama nyingine na kampuni ya Cowbell, hivyo hawapo tayari kuwaangusha.

"Sisi ndio timu pekee ya Ligi Kuu kutokea Mkoa wa Pwani, udhamini huu hautoshi kwa vile tunataka tufanye vizuri zaidi ya hapa, lakini mashabiki wanatakiwa watuunge mkono kupitia kununua jezi hizi," alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happiness Seneda aliyekuwa mgeni rasmi, alisema udhamini wa jezi umeongeza chachu ya mafanikio kwa Ruvu Shooting Ltd.

"Tunashukuru Cowbell kwa kuendelea kuwa nasi, ila tunayaomba makampuni mengine yaongeze uzito ili timu yetu ifanye vizuri."