Rais wa Fifa amtaja Mbwana Samatta

Dar es Salaam. RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino amesema anamsikia mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta lakini akasema ongezeni bidii Watanzania mtafika mbali na kuwa na wachezaji zaidi wa kulipwa duniani.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Infantino alisema kuwa wachezaji wa Tanzania wanaweza kufika mbali, lakini wakijituma na kusimamia misingi ya soka.

"Nimesikia kuna mchezaji wa Tanzania anachezea KRC Genk, lakini kama mkakati ukiwekwa, wachezaji wanaweza kufika mbali kwa kuwa nimeambiwa Tanzania kuna vipaji vingi vya soka."

Alisema pia kuwa maendeleo ya soka Tanzania yaweza kupatikana kwa Watanzania wenyewe kujipanga hasa katika kuucheza mpira, ujenzi wa miundombinu ya mchezo huo ikiwemo viwanja.

"Ninaamini kama wachezaji watajituma, watafuata maelekezo na utaratibu, Tanzania inaweza kufika mbali," alisema Infantino.

Alisema kuwa hawezi kuacha kuisemea Tanzania kwa kuwa anaona wanataka kufika mbali na kama Fifa, ataisaidia katika kufikia mafanikio.