Rais Infantino kutua na wajumbe 70 wa Fifa

Muktasari:

Ujumbe huo wa Fifa unakuja nchini kwa ajili ya kikao maalumu, huku Tanzania ikiwa nchi mwenyeji na itawakilishwa na wajumbe watatu akiwamo Leodegar Tenga ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo (BMT).

KUANZIA leo Jumanne Tanzania inatarajiwa kupokea wajumbe 70 ambao ni wanachama wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), watakaoanza kuingia leo huku Rais Gianni Infantino akitarajiwa kutua nchini kesho Jumatano.

Ujumbe huo wa Fifa unakuja nchini kwa ajili ya kikao maalumu, huku Tanzania ikiwa nchi mwenyeji na itawakilishwa na wajumbe watatu akiwamo Leodegar Tenga ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo (BMT).

Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema jana jijini Dar es Salaam, ajenda kuu ya mkutano utakaongozwa na rais wa Fifa ni kujadili soka la vijana, soka la wanawake na maendeleo ya pesa za Fifa wanazotoa kwa wanachama wao.

“Kwa kawaida kila nchi inatakiwa kuingiza wajumbe wawili ambao ni mtendaji mkuu wa TFF na rais wake, lakini pia Tenga naye atakuwepo kwa vile yeye ni mjumbe wa CAF.”

“Tumebahatika kupokea ugeni huo, kwani sisi ni miongoni mwa waumini wa soka la vijana, tunajua hakuna njia fupi ya kufikia mafanikio, hivyo tutatumia kikamilifu kikao hicho kwa ajili ya manufaa ya nchi,” alisema.

Naye Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema yeye ndiye atakayekwenda kumchukua rais wa Fifa katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro (atakakofikia) na kumpeleka Ikulu kusalimiana na Rais John Magufuli.

“Niweke wazi kazi yangu kwa siku hiyo, itakuwa ni kumchukua huyo mgeni kutoka Fifa katika hoteli aliyofikia na kumpeleka Ikulu kuzungumza na Rais wa Tanzania, mawili matatu, kisha ataendelea na ratiba zake, kwenye mkutano huo hata mimi siruhusiwi kuwepo.”