Prisons yaichapa Mwadui

Muktasari:

Mwadui imebaki katika nafasi ya 12 baada ya kucheza michezo 19 ikishinda mechi tatu tu hadi sasa

Mbeya. Kocha Mkuu wa Mwadui Fc ya Shinyanga, Ally Bizimungu ametoa sababu ya vijana wake kushindwa kutumia nafasi walizopata imechangia kufungwa kwao bao 1-0 na Tanzani Prison.

Prison ilipata bao pekee dakika ya 54 likifungwa kwa kichwa safi na nahodha wake Laurian Mpalile akiunganisha krosi iliyopigwa na Benjamin Asukile.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi uliochezewa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Kocha Bizimungu alisema vijana wake walijawa na presha kutokana na mwamuzi kuegemea upande Prison.

“Vijana wangu wamecheza mpira safi... Ila mchezo umeharibiwa na mwamuzi kwani hakuwa 'fair' hivyo imewafanya wachezaji wangu na presha. Kwa ufupi mwamuzi ndio kachangia ushindi wa Prison na si vinginevyo," alisema Kocha huyo.

Alisema wachezaji wake walipata nafasi nyingi, lakini baadhi walikosa kutokana na uamuzi wa mwamuzi kupuliza kipyenga hata sehemu isiyostahili.

Alisema hawakati tamaa licha ya kuwa ligi hiyo kuwa ngumu, lakini wanaendelea kujipanga na mechi zijazo.

Kocha Mkuu wa Prison, Mohammed Abdalah alisema ushindi alizopata ni muhimu kwake kwani zinazidi kumuweka kwenye bafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo.

Alisema mechi ni ngumu, lakini vijana wamepambana hadi kupata bao moja na ambalo limetufanya tuibuke na pointi tatu muhimu kwetu.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Ruvu Shooting imeichapa Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.