Posta yatangaza vita kwa Mahia, Leopards

Friday February 9 2018

 

By VINCENT OPIYO

Nairobi. KOCHA wa Posta Rangers, Sammy Pamzo Omollo amedokeza haogopi mabingwa wa KPL Gor Mahia na wa Ngao ya GOtv, AFC Leopards kwenye ushindani wa msimu huu.

Hata hivyo, Omollo anakiri kwamba vigogo hao pamoja na Sofapaka, Ulinzi Stars na Tusker watakua na upinzani mkali ila kikosi chake kipo tayari kupambana nao.

"Tumefanya sajili nzuri msimu huu kwamba, kila nafasi ina wachezaji wawili hivyo tunafanya bidii kuhakikisha tunafanya vyema zaidi kuliko mwaka jana," alisema Pamzo aliyeongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya nne msimu jana.

Posta walitoka sare ya 1-1 mechi ya kwanza wikiendi jana dhidi ya Ingwe na Jumapili hii wanamenyana na Tusker kwao Ruaraka.

"Mechi ya Leopards tulicheza vizuri tukapoteza nafasi za wazi. Cha kusikitisha hatukuvuna alama zote tatu, lakini tunalifanyia marekebisho tulipokosea ili akija Tusker tunamaliza mapema tu, " aliongeza Pamzo akisema atazikosa huduma za winga Danson Kago anayeugua.

Kiungo Peter Opiyo almaarufu Pinchez yupo fiti mazoezini na huenda akapewa nafasi ya kwanza kikosini kwa mujibu wa Pamzo.