Polisi, Coastal Union kama ubaya ubaya tu

Arusha: Polisi Tanzania itakuwa na kazi moja kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa ligi daraja la kwanza (FDL) utakaopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi kesho, Jumamosi.

Coastal inayoongoza Kundi B tayari imewasili Mkoani Kilimanjaro ikiwa na kikosi kamili cha wachezaji huku Kocha Mkuu Juma Mgunda alisema wachezaji wote wapo katika hali ya ushindani kuelekea katika mchezo huo.

“Ushindi ni lazima kwani tuna kila sababu ya kushinda mchezo huo kwasababu tumewajua wapinzani wetu udhaifu wao na tutatumia nafasi hiyo kuwaangamiza nyumbani kwao,” alisema Mgunda.

Hata hivyo, kocha msaidizi wa Polisi Tanzania, John Tamba alisema timu hiyo yenye maskani yake Moshi Mkoani Kilimanjaro imeeleza kujipanga kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo ili kurudi kileleni.

 Maafande hao wapo nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi B’ ikiwa na pointi 20, huku wapinzani wao Wagosi wa Kaya wakiongoza kundi hilo ikiwa na pointi 21 sawa na JKT Mlale itakayoumana na Polisi Dar Jumanne ijayo.

“Tunakwenda kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa kwa kudhibiti hujuma za aina yoyote zitakazoweza kujitokeza kwa kuzingatia rekodi ya mpinzani wetu na wachezaji wanapaswa kuwa na nidhamu ya hali ya juu” alisema Tamba.

 

Aliongeza kuwa timu yao ndio bora kwa sasa na tunapenda kuona mwenye uwezo mkubwa uwanjani ndio ashinde badala ya watu kuja na matokeo mfukoni jambo ambalo halitakubalika kwa namna yoyote ile hiyo sio picha nzuri kimichezo.