Pointi tatu za Sadick zaibeba JKT RBA

Dar es Salaam. Nyota wa JKT, Baraka Sadick amesema kujituma ndio siri iliyomfanya kufunga pointi tatu mara 10 kwenye mchezo wao uliopita wa RBA dhidi ya Tanzania Prisons.

JKT ikiongozwa na chipukiziSadick ilikuwa moto wa kuotea mbali kwenye mchezo huo ambao waliibuka na ushindi wa pointi 95-66.

“Nilikuwa kwenye kiwango bora, nimekuwa mtu wa kufanyia mazoezi ile mitupio ya mbali ambayo inathamani ya jumla ya pointi tatu, nashukuru Mungu kwa kuisaidia timu yangu kushinda.

“Hatujapoteza mchezo hata mmoja, tupo nafasi ya tano ni kutokana na kuwa nyuma michezo miwili. Nitaendelea kujituma ili kuwa kwenye kiwango bora zaidi,” alisema nyota huyo.

Sadick aliweka rekodi kwenye mchezo wao uliopita wa RBA kwa kufunga jumla ya pointi 41 ambazo zitasimama kama idadi kubwa zaidi ya  pointi ambazo zimefungwa tangu kuanza kwa msimu.

RBA itaendelea kutimua tena vumbi leo kwenye uwanja wa  Bandari, Kurasini kwa Vijana kuchuana na UDSM Insider na Kigamboni itacheza na Magnet.