Pawasa anayo dawa ya Simba kuing’oa Al Masry

Muktasari:

Pawasa ambaye alikuwepo kwenye kikosi cha Simba kilichoiondosha Zamalek mwaka 2003, alisema wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi wanatakiwa wawe makini na mwamuzi wa mchezo huo kwani mara nyingi ndio huzitoa timu zetu mchezoni.

MARA Paap, Al Masry hawa hapa. Wakati mashabiki wa Simba wakiingia mchecheto baada ya kuangukia na Al Masry kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, beki wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa amewatuliza.

Pawasa ambaye alikuwepo kwenye kikosi cha Simba kilichoiondosha Zamalek mwaka 2003, alisema wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi wanatakiwa wawe makini na mwamuzi wa mchezo huo kwani mara nyingi ndio huzitoa timu zetu mchezoni.

“Katika mechi kama hizi marefa wanakuwa makini sana, kikubwa Simba wacheze kwa nidhamu kubwa sana wakiwa hapa na hata ugenini, filimbi kwao inatakiwa iwe ya kusimamisha mpira tu, lakini wakianza kulalamika kwa vitu vidogo kwa refa itawagharimu,” alisema beki huyo wa kati wa zamani wa kimataifa wa Tanzania.

Pawasa aliongeza, mechi hizo zinakuwa na maana kubwa sana kwa wachezaji kwani huwa wanatumia fursa ya kujitangaza ili waweze kuuzika kwenye timu za nje.

“Zamani sisi ilikuwa ngumu sana kuondoka hata kama timu ikitokea inakuhitaji, lakini hivi sasa klabu zimefunguka zinawachia wachezaji ili wajenge timu bora ya taifa,” alisema.

Hivyo akaitaka Simba isiingiwe na mchecheto kwa sababu kama watajipanga wanaweza kuwapiga El Masry ndani na nje na kujiweka pazuri kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho.

Simba imerudi kimataifa tangu ilipocheza mara ya mwisho mwaka 2013 na imetinga raundi ya kwanza kwa kuing’oa Gendarmerie ya Djibouti kwa mabao 5-0.