Pamba FC, Toto kupeana hukumu ya mwisho

Muktasari:

Pamba FC ina pointi 12 huku Toto Africans ikiwa na pointi saba, hivyo kama Toto itashinda itafikisha pointi 10 na kuiweka TP Lindanda katika wakati mgumu ikiwa imebaki na michezo miwili kabla ya ligi kumalizika.

Mwanza. Pamba FC ‘TP Lindanda’ itawavaa ndugu zao wa Toto Africans leo Jumapili kwenye Uwanja wa Nyamagana, katika mchezo utakaoamua hatima yao ya kubaki katika Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Pamba FC ina pointi 12 huku Toto Africans ikiwa na pointi saba, hivyo kama Toto itashinda itafikisha pointi 10 na kuiweka TP Lindanda katika wakati mgumu ikiwa imebaki na michezo miwili kabla ya ligi kumalizika.

Kocha wa Pamba Venance Kazungu alisema hawatawadharau Toto Africans katika mchezo huo kwa kuwa ili kuwa salama katika janga la kushuka daraja ni lazima washinde mchezo huo.

“Hii ni kama fainali yetu kama tunataka tusiwe katika nafasi mbaya ya kushuka daraja msimu ujao ni lazima tupate ushindi katika mchezo huu,”alisema Kazungu.

Kazungu alisema mechi zilizobaki ni ngumu dhidi ya Alliance  kabla ya kwenda mkoani Tabora kumalizana na Rhino Rangers kwenye mchezo wa Kundi C.

“Ukiangalia baada ya kucheza na Toto Africans tutakuwa tumebakisha mechi mbili ambazo zote ni ngumu tutacheza na Alliance kisha tutamaliza na Rhino Rangers,”alisema kocha huyo.