Ozil ampasua kichwa Wenger

LONDON, ENGLAND. Kocha, Arsene Wenger amesema hafahamu kwanini Mesut Ozil bado anaendelea kuumwa, lakini anaamini atakuwa fiti itakapofika Jumapili ili kukipiga na Manchester City kwenye fainali ya Kombe la Ligi.

Ozil alikosa mazoezi ya siku mbili na jambo hilo limewafanya Arsenal kuwa na mashaka makubwa kwamba huenda akakosa pia fainali hiyo muhimu ya kuwapata walau taji ndani ya msimu huu. Ni mara ya nne msimu huu Ozil akiwa nje ya uwanja kutokana na kuumwa na Wenger alidai kwamba staa huyo ana shida katika mfumo wake wa damu.

Wenger alisema: "Mfumo wake wa damu unashida na sijui kwanini. Tunaamini anaweza kuwa vizuri baada ya kupatiwa matibabu. Alifanya mazoezi Ijumaa na Jumamosi, lakini tangu Jumatatu yupo kitandani. Nadhani atakuwa fiti Jumapili."