Okwi ndani ya nyumba Dar

Sunday January 14 2018

 

By MWANDISHI WETU

UZITO wa mechi ya Singida United umeilazimisha klabu ya Simba kutumia nguvu ya ziada kumrejesha nchini staa wao, Emmanuel Okwi ili aongeze nguvu katika mchezo huo ambao utatoa taswira ya mbio za ubingwa msimu huu.

Okwi ambaye amekuwa nje ya uwanja tangu mwishoni mwa Novemba akiuguza majeraha ya enka, alitarajiwa kurejea nchini usiku wa jana ili ajiunge na wenzake kambini mjini Morogoro leo Jumapili.

Mmoja wa watendaji wa Simba alilihakikishia Mwanaspoti kuwa Okwi atakuwepo kwenye mchezo huo wa Alhamisi kwani tayari amepona majeraha yake hayo na jana usiku alikuwa njiani kurejea Dar es Salaam.

Staa huyo mwenye mabao manane Ligi Kuu jana jioni alizungumza na mashabiki wake kupitia mtandao wa Instagram na kuwahikikisha kuwa amepona na yupo tayari kurejea mzigoni.

Viongozi wa Simba jana jioni walishindwa kuthibitisha taarifa za ujio wa staa huyo, lakini Mwanaspoti lilijiridhisha pasi na shaka kuwa alikuwa safarini kurejea nchini na ataungana na wenzake kabla ya mchezo huo.

“Okwi yupo fiti na ataungana na wenzake kabla ya mchezo wa Singida. Tumemrejesha ili kuongeza nguvu kwenye mchezo huo,” alisema mmoja wa viongozi wa Simba aliyeomba hifadhi ya jina lake.