Okwi, Chirwa ni pacha, ila kila mtu lwake

HUKO mitaani kwa sasa kuna hadithi mbili zinaendelea. Hizi zinawahusu mastaa wa Simba na Yanga, Emmanuel Okwi raia wa Uganda na Mzambia Obrey Chirwa.

Mastaa hao wote wamekuwa na vitendo vya utovu wa nidhamu. Okwi alipotelea kwao Uganda na kushindwa kurejea kwa wakati kama ruhusa yale ilivyoelekeza.

Alitakiwa kurejea Januari 10, lakini akarudi siku sita baadaye. Tena kocha wake, Masudi Djuma alitaka arejee wakati wa Sikukuu ya Mwaka Mpya, lakini ikashindikana. Huyo ndiye Okwi, mfalme wa Simba.

Hadithi nyingine ni ya Chirwa. Huyu aliaga kuwa anakwenda kwao Zambia, lakini akatokomea moja kwa moja. Baadaye akaonekana akilima matikiti. Baadaye akaonekana akipalizi mahindi.

Mwishowe akarejea na kujiunga na timu huko Zanzibar ilipokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.

PACHA TOFAUTI

Utofauti wa Okwi na Chirwa ukaanza kuonekana huko. Pamoja na utovu wa nidhamu, wote walipewa vipaumbele na kuchezeshwa kwenye mechi zilizofuata.

Hakuna kiongozi wa timu aliyewanunia kwani, ndiyo mastaa wa timu zao. Okwi na Chirwa wakisema, viongozi wanasikiliza.

Bahati mbaya kwa Chirwa ni kwamba kurejea kwake hakukuwa na neema sana kwa Yanga. Kwanza, siku chache baada ya kurejea alisimamishwa kucheza mechi tatu za Ligi Kuu kwa vitendo vya utovu wa nidhamu alivyofanya kwenye mechi dhidi ya Prisons.

Pili, aliigharimu Yanga nafasi ya kutinga fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya kupiga penalti ‘nyepesi’ iliyodakwa kirahisi na kipa wa URA.

Okwi kwa upande wake alihitaji dakika 24 tu uwanjani kuisaidia Simba kushinda mabao 4-0 dhidi ya Singida United. Okwi alifunga mabao mawili ndani ya dakika sita tu katika mchezo huo wa Alhamisi iliyopita.

TAKWIMU ZAO

Chirwa hakuwa hodari sana wa kufunga pindi aliposajiliwa na Yanga mwaka 2016, lakini mwaka jana alifanya kazi kubwa na kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu.

Kiwango bora cha Chirwa, Saimon Msuva na Amissi Tambwe katika mechi za mwisho za Ligi Kuu ndicho kilichoipa taji Yanga iliyokuwa ikipelekwa puta na Simba.

Msimu uliopita alifunga mabao 12 kwenye Ligi Kuu na mengine matano kwenye Kombe la FA, yote akifunga kwenye mchezo mmoja.

Msimu huu Chirwa ndiye kinara wa mabao ndani ya Yanga akiwa amefunga mara sita. Ndiye mchezaji pekee aliyefunga hat trick Ligi Kuu, akifanya hivyo dhidi ya Mbeya City.

Okwi kwa upande wake ana historia kubwa na Simba. Alifunga mabao 12 wakati Simba ikitwaa taji lake la mwisho mwaka 2012. Msimu huo alitangazwa kuwa mchezaji bora wa kigeni.

Msimu wa 2014/15 aliporejea Simba kwa mara ya pili alifunga mabao 10 na kuwa mchezaji aliyeifungia timu hiyo zaidi kwa msimu huo.

Mwaka huu Okwi amerejea akiwa moto zaidi kwani katika mechi 13 tu zilizochezwa mpaka sasa, amefunga mabao 10. Pengine mambo mengine mazuri yanakuja.

NIDHAMU NGOMA DROO

Wachezaji hawa wana tabia zinazoshabihiana hasa kwenye upande wa nidhamu. Ila Chirwa ni kama amezidi kwani ni kama ana visa na kisirani.

Chirwa amewahi kugoma akishinikiza kupewa malipo yake ndani ya Yanga, tena wakati huo timu yake ikijikabiliwa na mchezo muhimu wa marudiano dhidi ya MC Alger ya Algeria.

Chirwa ameonyesha pia usumbufu pindi alipokwenda kwao kwa awamu hii. Pia aliwahi kumpiga Mpigapicha wa kampuni ya New Habari.

Kwa upande wa Okwi, tatizo lake kubwa ni pindi anapokwenda kwao kwani kurejea kwake ni majaliwa. Amekuwa akifanya hivyo kila wakati anapokuwa Msimbazi.