Nyoshi-Nifulie mimi?Aaaah wapi

Muktasari:

Rais huyo wa zamani wa Bendi ya FM Academia, Nyoshi asema wasifikiri mwanamuziki wa dansi akipanda jukwaani ndio vyuma vimekaza.

Dar es Salaam. Kiongozi na Rais wa Bendi ya Bogos, Nyoshi El Saadat amewapuuza baadhi ya watu wanaosema vyuma vimekaza na amejishusha thamani yake baada ya Jumapili iliyopita kupanda katika jukwaa la Bendi ya Dar Musica Original iliyokuwa inapiga kwenye ukumbi wa Meeda Sinza.

Nyoshi aliyasema hayo baada ya kuona maoni ya Meneja wa Twanga Pepeta, Hassani Rehani kwenye kipande cha video cha MCL Digital kilichorushwa katika kundi moja la Whatsapp la muziki wa dansi ikimwonyesha akiimba katika jukwaa la Dar musica.

Rehani kwenye maoni yake hayo aliandika 'Nyoshi anajishusha sasa au vyuma vimekaza?'.

Baada ya kuona maoni hayo Nyoshi alisema ameingia katika ukumbi wa Meeda akiwa kama mpenda burudani kama mashabiki na wadau wengine na akiwa hapo alikaribishwa jukwaani na mwimbaji wa bendi hiyo, Jado, ndipo alipohoji, je angekataa?au yeye siyo mwananuziki?

"Nimeshangazwa sana kwa kweli na baadhi ya watu kutoa komenti kuwa sikupaswa kupanda jukwaa la Dar Musica, hivi mimi nimekaribishwa, ina maana ningekataa au mimi nishakuwa sio mwanamuziki? Kiukweli huku ni kuvunjana moyo kwani kumbe kuna watu hawapendi mshikamano na ushirikiano," alisema Nyoshi.

Rais huyo wa zamani wa Bendi ya FM Academia, Nyoshi aliongeza "Wasifikiri mwanamuziki wa dansi akipanda jukwaani ndio vyuma vimekaza, hiyo mimi nakataa kabisa, yaani ni moja tu ya njia ya kusapotiana

"Ila naomba wafahamu tu, mimi vyuma havijakaza kama wanavyodai, kwani ningekuwa na njaa nisingekaa benchi miezi saba au minane sijaenda kuomba kazi popote na sijaenda kwenye bendi ya   mtu, nimetumia muda wote kuandaa bendi yangu mpya ya Bogos na ndio maana huwa na msimamo," alisema Nyoshi.

Mbali na hiyo Nyoshi alisema wanamuziki kualika katika jukwaa sio kitu cha kushangaza kwani hata huko nje ya nchi wenzetu wanafanya hivyo akitolea mfano Mwanamuziki JB Mpiana alipomwalika Ferre na Heritier, sasa iweje yeye akikaribishwa ionekane vyuma vimekaza?

Alisema pia amefanya hivyo kama njia ya kuurudisha kwenye chati muziki wa dansi kwani kwa sasa umeshuka.

Mwanaspoti halikuishia hapo, liliweza kupiga stori na Hassani Rehani na alisema aliandika hivyo kwa kuwa Nyoshi ni Brand kubwa na hakupaswa kupanda jukwaa la bendi ya Jado kwani anashusha thamani yake ikiwa bado hajazindua bendi yake.

"Akipanda panda ovyo tutasema anatafuta tunza ili kukidhi mahitaji ya sasa wakati hana kazi," alisema Rehani kwa maandishi huku akisisitiza kuwa vyuma vimekaza.

Mwanaspoti lilimshuhudi Nyoshi akiingia ukumbini Meeda na kuketi katika kufuatilia onyesho la bendi hiyo, ndipo mashabiki wa muziki walipomwona wakaanza kumfuata huku wakitaja jina lake Rais Nyoshi... Rais Nyoshi... Rais Nyoshi wakati bendi hiyo ikitumbuiza jukwaani. Makelele yalipozidi ndipo Jado akaamua kumkaribisha Nyoshi apande jukwaani na kuwasalimia mashabiki.