Nyamagana kama utani wabomolewa

Muktasari:

  • Hata hivyo, la kufurahisha, bomoa bomoa katika uwanja huo uliowahi kuchezewa pambano la kihistoria la Simba na Yanga mwaka 1974 na Simba kulala 2-1, haitaikumba eneo la kuchezea, bali ni ukuta wa uwanja huo.

UKIWA hauna hata muda mrefu tangu ulipozinduliwa baada ya kukaa muda mrefu bila kukamalishwa ukarabati wake wa kuwekwa nyasi bandia, uwanja wa Nyamagana wenye historia kubwa kwa soka la Tanzania, umebolewa.

Hata hivyo, la kufurahisha, bomoa bomoa katika uwanja huo uliowahi kuchezewa pambano la kihistoria la Simba na Yanga mwaka 1974 na Simba kulala 2-1, haitaikumba eneo la kuchezea, bali ni ukuta wa uwanja huo.

Ukuta wa uwanja huo uliopo jijini hapa umekuwa miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na operesheni ya bomoa bomoa kupisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge) unaokaribia kuanza nchini.

Awali uwanja huo ulikarabatiwa na kuwekwa nyasi bandia mwaka juzi tu, lakini sasa ukuta wake unatakiwa kubomolewa na Kampuni hodhi ya rasilimali za reli nchini (Rahco), ikiwa ni utekelezaji wa zoezi la kubomoa nyumba zilizojengwa ndani ya mita 15 hadi 30 ya njia ya reli.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba hivi karibuni alisema mbali na Nyamagana, ubomoaji huo utaathiri maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba na taasisi.

“Taasisi zitakazoathirika ni pamoja na ukuta wa Uwanja wa Nyamagana, ukuta wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Kiwanda cha Samaki cha Vicky Fish nyumba za ibada na kadhalika,” alisema.

Akizungumzia ubomoaji huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo alisema huo ni utaratibu ambao ulitangazwa mapema, hivyo wanaupokea kama ulivyo.

Alisema wao kama MZFA, wanawaomba wamiliki wa uwanja huo, ambao ni Halmashauri kuhakikisha wanakarabati haraka ukuta huo ili kulinda mali zilizomo ndani.

Baadhi ya wadau wa soka jijini hapa, Ahmad Hussein na Juma Mohamed walisema zoezi hilo ni sahihi kwani kila kitu kina utaratibu wake.

“Ni sahihi kwa sababu ukisema uwanja usiingiliwe unakuwa umependelea upande mmoja. Makanisa, misikiti, ofisi za watu zivunjwe iweje uwanja? Lazima sheria iguse kote,” alisema Hussein.

Hata hivyo, baada ya ubomoaji huo viongozi wa MZFA walikuwa wakihangaika kutafuta maturubai na mavero kufunika eneo hilo ili watazamaji wa mechi ya Toto Africans na Oljoro wasipenyeze ndani bila kulipa viingilio.