Ngoma kwa daktari tena

Muktasari:

  • Mkwasa ambaye ni mchezaji na kocha wa zamani wa timu hiyo, alisema muda wa Ngoma kuwa nje akiuguza majeraha yake ulimalizika tangu Januari 10

MASHABIKI Yanga wameanza kuingiwa wasiwasi juu ya hatma ya mshambuliaji wao, Donald Ngoma, lakini mtendaji wa klabu hiyo, Charles Mkwasa,  amesema jambo.

Mkwasa ambaye ni Katibu Mkuu, alisema taarifa aliyonayo ni kwamba muda ambao Ngoma alitakiwa awe nje ya uwanja umeshapita na sasa anatakiwa kuanza mazoezi.

Mkwasa ambaye ni mchezaji na kocha wa zamani wa timu hiyo, alisema muda wa Ngoma kuwa nje akiuguza majeraha yake ulimalizika tangu Januari 10 ambapo sasa hatma yake ipo kwa daktari bingwa anayemtibu kutoa ruhusa ya kucheza ama la.

Alisema Ngoma amerudi kwa daktari anayemtibu kupewa ratiba kamili ya aina ya mazoezi anayotakiwa kufanya kabla ya kurudi kujiunga na wenzake na kuendelea na ratiba ya makocha wa kikosi chao.

“Ninachojua kuhusu Ngoma ni hicho. Anachotakiwa kufanya ni kuchukua mwongozo wa mazoezi kutoka kwa daktari aliyekuwa akimtibu ili aanze kujifua,” alisema.