Ndio! Mkizubaa tu mjue mtaumia

Muktasari:

Ruvu itaikabili Yanga katika mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa, ikiwa na rekodi mbaya mbele ya vijana wa Jangwani, lakini kwa matokeo ya mechi iliyopita ya Yanga imewapa mzuka wa kuwatibulia.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina bado hajapata kibali cha kuendelea na kazi Jangwani, lakini hiyo sio ishu ya kuwazuia vijana wake kufanya kweli wakati wakiwakabili Ruvu Shooting katika moja ya mechi za Ligi Kuu Bara leo Jumapili.

Ruvu itaikabili Yanga katika mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa, ikiwa na rekodi mbaya mbele ya vijana wa Jangwani, lakini kwa matokeo ya mechi iliyopita ya Yanga imewapa mzuka wa kuwatibulia.

Yanga ililazimishwa suluhu katika mechi yao iliyopita dhidi ya Mwadui na kuifanya isalie katika nafasi ya tano na alama 22, kitu ambacho kama leo haitajipanga vyema huenda wakazidi kujiweka pabaya katika mbio za kutetea taji.

Asubuhi ya jana Jumamosi, Yanga ilipiga tizi kwa muda mfupi kwenye Uwanja wa Uhuru, huku wachezaji wao wakionekana kuwa na morali wa kusaka ushindi pengine kutokana na kitimoto walichowekwa juzi Ijumaa na mabosi wao.

Nyota wa Yanga wanafahamu kama hawatajipanga vyema na kupoteza mchezo huo ama kupata matokeo ya sare, yatazidi kuiweka timu yao katika nafasi mbaya na kuongeza pia pengo la pointi baina yao na watani zao Simba wanaoongoza msimamo kwa alama 29. Pointi saba zaidi dhidi ya zile ilizonazo Yanga. Simba yenyewe ipo mjini Bukoba na kesho Jumatatu itashuka Uwanja wa Kaitaba kuvaana na wenyeji wao Kagera Sugar wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 kwenye uwanja huo msimu uliopita.

Matokeo hayo ya kipigo ndiyo yaliyoibua sakata la kadi tatu za njano za Fakhi Mohammed, Simba ikitaka kupewa ushindi wa mezani na ilipewa na Kamati ya Saa 72 kabla ya ushindi huo wa dezo kutenguliwa na kutoa nafasi kwa Yanga kutetea taji, licha ya watani zao kukimbilia FIFA kutaka ipewe ubingwa.

Yanga inafahamu, mbali na Simba inayozidi kuwaacha, pia kuna Azam ambayo jioni ya leo nao watakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine, kuvaana na Prisons inayoipumulia vijana wa Jangwani nyuma yao na alama zao 21.

Kadhalika kuna Singida United waliopo juu yao na alama zao 23 licha ya kuchezea kichapo cha mabao 4-0 katika mechi yao iliyopita dhidi ya Simba na kesho nao watashuka uwanja wa ugenini kuvaana na Majimaji ugenini mjini Songea.

 

Msikie Cannavaro

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ anajua hali walizonazo mashabiki wa Yanga hasa kutokana na kufanya vizuri kwa watani zao na kuwatuliza kwa kuwaambia wasiwe na wasiwasi, kwani leo lazima Ruvu wale nyingi tu.

Cannavaro alisema Ruvu ni mwanzo wa kuonyesha kasi yao kama ya misimu iliyopita ya kugawa dozi na kuwapa faraja mashabiki wao ambao wamekuwa hawana amani mitaani kisa Simba kufanya vyema katika mechi zao.

Akizungumzia nafasi ya ubingwa kwao alisema bado wana nafasi kubwa ya kuweza kuchukua, kutokana na pointi ambazo wapinzani wao wamewazidi, kikubwa ni kupata matokeo katika michezo iliyobaki.

“Ubingwa tunautaka, hatujakata tamaa sisi hata kidogo, wapinzani wetu wametuzidi pointi saba tu na bado kuna michezo mingi iliyobaki katika ligi, kwa nini tukate tamaa mapema?” alihoji Cannavaro mchezaji aliyeichezea Yanga kwa muda mrefu kuliko yeyote ndani ya kikosi hicho.

Ruvu nao wabishi

Kocha Mkuu wa Ruvu, Abdulmutik Haji ‘Kiduu’ alikiri timu yao ipo katika wakati mgumu msimu huu, pia ina rekodi mbaya mbele ya Yanga, lakini katu  hawatakubali kufungwa kirahisi na wapinzani wao wanaowaheshimu.

Alisema licha ya mechi hiyo kupigwa Taifa, lakini bado wanaamini watapambana kusaka matokeo mazuri ili kujiweka pazuri katika msimamo kabla  kusubiri kumaliza mechi za duru la kwanza kujitathmini kwa duru la lala salama.

Tatizo rekodi

Licha ya Ruvu kutamba kutaka kuibana Yanga, lakini rekodi zinawaangusha mbele ya wapinzani wao kwani mara nyingi wamekuwa wakichezea nyingi tu.

Rekodi zinaonyesha kuwa, msimu wa 2010/11 Ruvu walianzishiwa kichapo baada ya kupata kipigo cha mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Idd Mbaga na Jerry Tegete  katika duru la kwanza kabla ya kulala tena 1-0 kwa bao la Tegete.