Nani anauzwa, nani anabaki!

Muktasari:

Lakini, hilo la kumwaandama kocha Wenger linawaacha vipi wachezaji wa timu hiyo? Kwa viwango vinavyoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo, hakuna ubishi mwisho wa msimu itakapohitajika kufanyika mabadiliko, basi si kocha tu wa kuondoka, bali kuna wachezaji kibao wanaopaswa kufuatana na kocha huyo kuelekea mlango wa kutokea huko Emirates.

LONDONENGLAND. VIDOLE vyote ananyooshewa kocha Arsene Wenger. Anashutumiwa na kulazimishwa aondoke, abwage manyanga kwenye kuinoa Arsenal hasa kutokana na matokeo ya hivi karibuni yanavyovunwa na timu hiyo.

Lakini, hilo la kumwaandama kocha Wenger linawaacha vipi wachezaji wa timu hiyo? Kwa viwango vinavyoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo, hakuna ubishi mwisho wa msimu itakapohitajika kufanyika mabadiliko, basi si kocha tu wa kuondoka, bali kuna wachezaji kibao wanaopaswa kufuatana na kocha huyo kuelekea mlango wa kutokea huko Emirates.

MAKIPA

Petr Cech

Kipa, Cech analaumiwa kwa kipigo cha Brighton. Unakumbuka yale maneno ya Homer Simpson aliyomweleza baba yake, “Umefanya mambo mengi sana mazuri, lakini kwa sasa umeshakuwa mzee na mtu mzee hana faida tena.”

Maneno hayo yanaelezwa kwamba kumfaa kabisa kipa Cech, ambaye kwa sasa anaonekana hana jipya analoweza kuifanya Arsenal katika harakati zake za kujinasua. AUZWE.

David Ospina

Unapokuwa kipa wa chaguo la pili kwa muda mrefu ni suala la uamuzi wako mwenyewe kuendelea kubaki kwenye hali hiyo hiyo au kwenda kwenye timu ambayo itakuwa nafasi ya kucheza. Kipa Ospina amekuwa na imani kwamba, huenda akawa chaguo la kwanza wakati Cech atakapoondoka kwenye kikosi hicho. Lakini, kwa Arsenal kubaki na Ospina hawatakuwa na uhakika wa usalama wao, wanahitaji kuwa na kipa wa kiwango cha David De Gea au Ederson. AUZWE.

MABEKI

Laurent Koscielny

Mwepesi na mwenye akili ya mpira. Koscielny amekuwa beki wa kati anayefahamu vyema kujipanga anapokuwa ndani ya uwanja na hakika alikuwa kisiki kisichopitika kwenye kikosi cha Arsenal. Lakini, kiwango cha sasa cha mshambuliaji huyo kimekuwa tofauti kabisa ametokea kuwa shujaa hadi kufikia sasa akionekana kuwa beki wa hovyo hivyo. Kimsingi, Arsenal inahitaji kutafuta beki mwingine wa kati na kuachana na Koscielny. AUZWE.

Rob Holding

Hakika si beki wa kumtegemea na si beki mwenye kiwango cha kuichezea timu kubwa kama Arsenal inayokabiliwa na mashindano kibao ndani ya msimu mmoja. Holding inawezekana kuwa ni beki mwenye kipaji, lakini kitu ambacho Arsenal inapaswa kukifanya basi ni kumtoa kwa mkopo aende akapandishe kiwango chake na kisha kurudi kwenye timu hiyo kwa sababu kimsingi, Arsenal haipaswi kuwa timu ya majaribio. ATOLEWE KWA MKOPO.

Nacho Monreal

Kwa namna alivyoibuka na kuanza kufunga mabao msimu huu ni kitu kinachoonyesha kwamba, Monreal bado anastahili kupata muda zaidi wa kuendelea kuichezea Arsenal. Sawa umri wake ni miaka 32, lakini Mhispaniola huyo bado hajachoka na kiukweli amekuwa msaada mkubwa kwa timu ya Arsenal kwa wakati huu. Anahitaji kubaki kwa sababu safari lazima kuwa na mtu mzima. ABAKI

Shkodran Mustafi

Wakati wa dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwaka jana, mambo yalionekana wazi kwamba kocha Wenger alikuwa akisukumia Mustafi kwenda Inter Milan. Maisha yake ya siku za kwanza kwenye kikosi cha Arsenal yalikuwa mazuri na kuonekana kama vile Arsenal wameshamaliza shida ya mabeki, lakini tangu wakati huo, Mjerumani huyo amebadilika na kuwa mchezaji wa kawaida sana si wa thamani ya Pauni 35 iliyopita iliyotumika kumsajili miezi 18 iliyopita. AUZWE

Calum Chambers

Ameshatolewa kwa mkopo, lakini Chambers si aina ya mabeki ambao unadhani watakuwa na msaada kwenye kikosi cha Arsenal kama watarudisha kwenye kikosi hicho. Kiwango alichokuwa akikionyesha Southampton kilikuwa na matumaini, lakini kiukweli, Chambers ameshindwa kumudu umaarufu wa kuchezea timu kubwa kama Arsenal na hivyo si aina ya wachezaji wanaopaswa kuitumikia Arsenal kwa kipindi hiki kigumu. AUZWE.

Hector Bellerin

Ni mmoja wa wachezaji wachache kwenye kikosi cha Arsenal cha sasa ambao, wanaweza kwenda kwenye timu nyingine kubwa na kupata nafasi ya kucheza. Bellerin kiwango chake kinakuwa kutokana na timu inavyokuwa kwa sababu yeye bado kijana mdogo na hivyo, anahitaji kujengwa kimsingi. Barcelona kuna wakati walihitaji huduma yake na hakika Arsenal hawapaswi kupomteza beki wao huyo wa pembeni, atawasaidia. ABAKI.

Sead Kolasinac

Usajili wa bure kabisa ulionaswa na kocha Arsene Wenger kutoka Bundesliga. Maisha yake huko Emirates yalianza vyema kabisa kabla ya kushuka kiwango chake na kuonekana kuwa mchezaji wa kawaida tu kwenye kikosi hicho cha Arsenal. Hata hivyo, Kolasinac shida yake ilikuwa majeruhi na kama atakuwa fiti ni mchezaji ambaye hakika Arsenal haipaswi kupoteza huduma yake kutokana na kile anachokifanya ndani ya uwanja. ABAKI.

VIUNGO

Henrikh Mkhitaryan

Ana wiki chache tu kwenye kikosi cha Arsenal, hivyo ni mapema kumhukumu kwa kile kinachoendelea kwenye timu hiyo. Ni wazi kabisa Mkhitaryan ni moja ya wachezaji mahiri walipo kwenye kikosi cha Arsenal ambao, wanapaswa kuendelea kubaki hapo kwa muda mrefu. Kitu kibaya kwa mchezaji huyo ni kwamba, sasa amepoteza mechi nne kati ya tano alizoitumikia Arsenal kwenye Ligi Kuu England, wakati huko Man United alipoteza tano tu kwa mwaka mmoja na nusu. ABAKI.

Aaron Ramsey

Kama ikiendelea kubaki kama alivyo sasa, yaani kwa maana ya kama kocha Wenger akiondoka kuna mambo mengi ya kumfikiria kiungo Aaron Ramsey. Haifahamiki kama staa huyo ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho au ataondoka kutokana na ukweli kwamba, amekuwa mchezaji wa Wenger. Hata hivyo, kwa huduma ya ndani ya uwanja, Arsenal hawapaswi kumpoteza Ramsey hali itakuwa mbaya zaidi. ABAKI.

Jack Wilshere

Kwa kipindi hiki kigumu kwa mashabiki wa Arsenal kitu pekee ambacho wanakifurahia wanapokwenda kutazama mechi zao basi ni kumtazama Jack Wilshere anavyocheza soka lake. Hilo ndilo linalowapata faraja mashabiki wa timu hiyo kwa sasa licha ya kwamba, mkataba wake utafika tamati mwisho wa msimu na atakuwa huru kuondoka. Kitu kikubwa kitakachowapa faraja mashabiki wa Arsenal kama ataamua kumsainisha mkataba mpya Wilshere kabla ya msimu kumalizika ili kuhakikisha kiungo huyo anabaki Emirates. ABAKI.

Mesut Ozil

Huwezi kumpa mtu mkataba wa kumlipa mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki na kisha ndani ya muda mfupi tu kuamua kuachana naye. Hakuna namna nyingine kwa Arsenal bali ni kuendelea kubaki na kiungo wao wa Kijerumani, Mesut Ozil walau kwa msimu mmoja zaidi. Kwa wakati huu si mchezaji unayeweza kumzungumzia kwamba, ataondoka mwishoni mwa msimu huu kwa sababu ndiyo kwanza atakuwa anaanza kutumikia mkataba wake mpya. ABAKI.

Alex Iwobi

Kocha Wenger amekuwa akimpendelea kumpanga kwenye kikosi chake walau kuonyesha kwamba, kuna kitu anachoweza kukifanya. Hata hivyo, Iwobi ameshindwa kulipa fadhila hiyo kutoka kwa kocha wake na kucheza kwa kiwango cha hovyo sana. Umri mdogo unatajwa kuwa ni shida kwa sababu Iwobi ndiyo kwanza ana miaka 21, hivyo anahitaji muda zake wa kupevuka na kuwa mchezaji wa kutegemewa. ABAKI.

Santi Cazorla

Si kitu kinachovutia kukizungumzia. Pengine kiungo huyo Mhispaniola, Santi Cazorla kama angekuwa ndani ya uwanja akicheza, angehukumiwa tofauti. Majeruhi ya muda mrefu yamemfanya awe nje ya uwanja kwa kipindi kirefu na hivyo, haonekani tena kuwa na matumaini ya kurejea uwanjani hivi karibuni huku mkataba wake ukimalizika mwishoni mwa msimu huu. Kinachoonekana hapo ni kwamba Arsenal watakubali tu yaishe kuachana naye. AUZWE

Granit Xhaka

Wakati anatua kwenye kikosi cha Arsenal matumaini yalikuwa makubwa sana kwamba, sasa Wenger amemaliza tatizo la kiungo wa kati lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu. Lakini, matokeo yake mambo yamekuwa tofauti kabisa kwa sababu Xhaka ameshindwa kumaliza matatizo yaliyokuwa yakiikabili Arsenal kwa miaka yote na kuendelea kubaki vile vile. Arsenal inahitaji kiungo mpya wa kati, huyu Xhaka hawafai. AUZWE.

Ainsley Maitland-Niles

Ni mmoja wa wachezaji wanaonufaika na hali ngumu iliyopo kwenye kikosi cha Arsenal kwa sasa. Kushuka viwango kwa wachezaji wengi kwenye kikosi hicho kumemfanya kinda Maitland-Niles kupata nafasi ya kucheza na hadi sasa tayari ameshacheza mara 21 katika kikosi hicho cha Arsenal akijaribu kuvuna uzoefu na ukomavu wa mikikimikiki ya Ligi Kuu England. Bado kuna kitu kinachoweza kuvunwa kutoka kwake. ABAKI.

Mohamed Elneny

Labda kama kutakuwa na mpango wa kumbadili nafasi na kumtumia kama beki wa kati pindi Arsenal itakapohitaji kucheza fomesheni ya kutumia mabeki wa kati watatu. Lakini, hilo litafanyika kama tu timu hiyo haitakuwa siriazi kwenye kusaka matokeo chanya uwanjani. Kwenye kiungo, Elneny hana kitu kikubwa anachoweza kuipa ofa Arsenal, hivyo hata akiondoka hakuna kitakachokuwa kimepotezwa. AUZWE.

WASHAMBULIAJI

Alexandre Lacazette

Mambo si mazuri kabisa kwa fowadi Alexandre Lacazette. Tangu alipotua Arsenal upepo umekuwa tofauti na alivyokuwa huko Ufaransa. Lakini, imani ni kubwa kwamba mambo yatatulia na fowadi huyo atakuwa msaada kwenye kikosi hicho kama Wenger ataonyesha kumwaamini na kumpa muda wa kutosha wa kucheza ndani ya uwanja. Kwa Lacazette ni suala la kuaminika tu ni mchezaji anayeendelea kuhitajika Arsenal. ABAKI.

Pierre-Emerick Aubameyang

Ni wazi kabisa ni lazima abaki. Straika Aubameyang ndiyo kwanza ametua kwenye kikosi cha Arsenal kwanza bado hajazoea mfumo na kingine ni kwamba, amekuja katika kipindi ambacho morali ya timu ipo chini na hilo si jukumu lake peke yake kuweka hali ya mambo kuwa sawa. Kama ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho Auba atakuwa na maada mkubwa kwa timu na si staa ambao Arsenal wanapaswa kumhukumu kwa sasa. ABAKI.

Danny Welbeck

Haonekani kama kuna maajabu ya ziada anayoweza kufanya kwenye kikosi cha Arsenal kwa kipindi chote alichokuwa kwenye timu hiyo. Danny Welbeck ni mchezaji wa kiwango cha kawaida sana, wakucheza kwenye timu ndogo na si kubwa kama ilivyo kwa kiwango cha Arsenal. Hakuna ubishi kwamba alikuwa na bahati tu kuzichezea Manchester United na Arsenal kwenye ligi hiyo. AUZWE.