Mziki wa Yanga

Muktasari:

Township inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya kwao, itaifuata Yanga katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi hiyo mwezi ujao jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao baadaye huko Gaborone na mshindi atafuzu makundi.

SAWA, inawezekana ni kweli Yanga imepenya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama zali tu, lakini asikwambie mtu mziki wa vijana hao wa Jangwani umewatikisa wapinzani wao kutoka Botswana, Township Rollers.

Township inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya kwao, itaifuata Yanga katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi hiyo mwezi ujao jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao baadaye huko Gaborone na mshindi atafuzu makundi.

Wababe hao wa Botswana waliing’oa El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda nyumbani 3-0 na kupoteza ugenini 2-1, huku Yanga ikishinda nyumbani 1-0 na kulazimishwa sare ya 1-1 ugenini kwa St. Louis ya Shelisheli.

Wakati mashabiki wengi wa soka hasa watani zao Simba wakiibeza Yanga kwamba msimu huu imekuwa ya kuungaunga na isipoangalia inaweza kung’oka mapema, Kocha Mkuu wa Township, Nikola Kavazovic, presha imeanza kupanda.

Kocha huyo Mserbia amefichua kuwa awali alikuwa na presha kubwa kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano dhidi ya El Merreikh, lakini sasa nguvu zake zote zipo kwa Yanga ili kuanza kuwasoma.

Kavazovic amesema haijui vema Yanga, lakini kwa namna alivyopata wasifu wake, ni timu kali kutoka Afrika Mashariki na ina uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa, hivyo anaanza kuifuatilia kwa undani akisaka video zao.

“Sikutaka kuifikiria Yanga kabla ya mechi yetu ya El Merreikh, kwa sababu huwezi kuandaa msosi wa jioni wakati Sungura akiwa bandani, lakini kwa kuwa tumemchinja Sungura, tunaweza kuandaa msosi wetu,” Kocha huyo alinukuliwa na mtandao wa klabu hiyo.

“Nimeanza kuangalia video na kupata habari zote kuhusu Yanga na tutafanya maandalizi ya kutosha ili kufanya kweli katika mechi zetu na kuhakikisha tunatinga katika makundi.”

Kocha huyo alisisitiza wanataka kujiandaa vema zaidi kuliko ilivyokuwa kwa El Merreikh kwani Yanga ndio inayoweza kuwazuia au kuwapeleka makundi na kudokeza wamerudi nyumbani kujiandaa na mchezo wao wa fainali za Mascom Top 8 dhidi ya Orapa United kisha kuivaa BDF IX katika mechi ya Ligi Kuu kabla ya kuifuata Yanga.

Yanga kiroho safi

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina na baadhi ya nyota wake wameondoka Dar alfajiri ya leo Jumamosi kwenda Songea kucheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Majimaji wakisisitiza kutokuwa na presha yoyote.

Lwandamina alisema jana kuwa badala ya kuifikiria Township, mipango yake ni kuitengeneza timu kwa muda uliosalia ili kuwa na ushindani mkubwa na hata itakapovaana na wapinzani iwe na kazi rahisi.

Mzambia huyo alisisitiza anataka kumaliza mchezo hapa nyumbani badala ya kujipa presha kwenye mechi za ugenini kama ilivyokuwa dhidi St. Louis, huku akimtetea kipa Youthe Rostand juu ya madai aliifungisha timu.

“Tunajua tupo kwenye hatua ngumu, lakini kiu yetu ni kuona tunafuzu makundi, hivyo nawajenga vijana wangu tupate matokeo mazuri nyumbani kabla ya kumalizia kazi ugenini, hatuidharau timu yoyote, lakini hatukubali kupoteza,” alisema.

“Kuhusu Rostand ndiye aliyeiokoa timu ugenini, tangu baada ya gemu ya nyumbani nilimtoa kwenye mipango Ramadhani Kabwili baada ya kuwasoma St. Louis walitaka kupata matokeo kwa mipira iliyokufa na walipoona tumebadili kipa walipagawa na ndio maana walikuwa wakimchezea vibaya ili atoke,” alisema.

Yanga na Township zitavaana Machi 7 kabla ya kurudiana siku 10 baadaye na mshindi atafuzu makundi na anayeng’oka ataangukia Kombe la Shirikisho.