Mwamuzi ampiga ngwala mchezaji uwanjani

Muktasari:

Ni matukio machache sana ambayo waamuzi wamekuwa wakifanyia vurugu wachezaji wakati mechi inaendelea

Paris, Ufaransa. Mwamuzi Tony Chapron amefanya kioja katika mchezo wa Ligi Kuu Ufaransa, baada ya kumpiga teke beki wa Nantes Diego Carlos na kumpa kadi nyekundu wakati mchezo ukiendelea.

Tukio hilo lilitokea katika mchezo ambao Paris Saint Germain (PSG) ilishinda bao 1-0, lililofungwa na kiungo wa pembeni Muargentina Angel Di Maria.

Mwamuzi huyo ameishangaza dunia kwa kumpiga teke Carlos akimrudishia baada ya kuanguka alipogongana na beki huyo katika harakati za kuwania mpira.

Wakati mchezaji huyo akiwahi mpira, Chapron alikatiza mbele yake na kujikwaa katikati ya miguu yake kabla ya kupiga mwereka alipokuwa chini alijaribu kumrudishia ili amwangushe beki huyo.

Muda mfupi baada ya kuamka akionekana mwenye hasira alimpa kadi ya pili ya njano kabla ya kumlima nyekundu. Awali, Carlos alikuwa na jadi ya njano.

Tukio hilo limepamba vyombo vya habari duniani kwa kuwa halikuwa la kawaida na tayari Rais wa Nantes, Waldemar Kita, ametaka mwamuzi huyo afungiwe miezi sita.

Mbali na kumpa kadi nyekundu, mwamuzi huyo alitoa adhabu kuelekea langoni mwa Nantes kutokana na tukio hilo lilitokea dakika ya 90.

“Nimepokea meseji 20 kutoka kila kona ya dunia ikinieleza mwamuzi alifanya masihara. Unataka niseme nini, nikisema sana nitaonekana naingilia mamlaka za watu. Hii ni kashfa amempa kadi mchezaji ambaye hakuwa na kosa,”alisema kigogo huyo.

Kita alisema mwamuzi anatakiwa kuomba radhi kwa tukio hilo ambalo limeharibu taswira ya soka na amependekeza adhabu ya miezi sita itakuwa fundisho kwake.

Kigogo huyo alisema anasubiri kuona mwamuzi huyo atachukuliwa hatua gani kwa kosa hilo alilodai bila shaka hakutenda kwa kukusudia baada ya kuanguka.

“Naomba niwe mkweli, nadhani hakufanya kosa lile kwa makusudi. Sitaki kuamini alikusudia, angalau angeomba radhi, lakini kumpa kadi nyekundu, hakuwa makini sijawahi kuona tukio hili kabla,”alisema Kita.