Mudathir apewa kazi maalumu Singida

Muktasari:

  • Mchezaji Bora huyo wa Novemba mwaka jana, ameliambia Mwanaspoti kuwa kocha wao (Hans Pluijm) amewapa mbinu za mchezo mzima, lakini kwa upande wake amekabidhiwa jukumu la kulitawala dimba la kati ambalo Kagera hupenda kulitumia kupata matokeo

KIUNGO, Mudathir Yahya, wa Singida United, amefunguka kuelekea mchezo wao wa leo Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar akisema amepewa mbinu za kuweza kuwamudu viungo wa wapinzani wao ili kuhakikisha wanapata pointi zote tatu.

Mchezaji Bora huyo wa Novemba mwaka jana, ameliambia Mwanaspoti kuwa kocha wao (Hans Pluijm) amewapa mbinu za mchezo mzima, lakini kwa upande wake amekabidhiwa jukumu la kulitawala dimba la kati ambalo Kagera hupenda kulitumia kupata matokeo.

“Kocha ni mzuri katika mbinu, amenipa mbinu za kuweza kuwakabili viungo wa Kagera lakini pia mimi katika kuhakikisha napeleka mashambulizi ili kuweza kupata mabao ambayo yatatufanya tupate ushindi ugenini,” alisema.

Akimzungumzia kiungo wa Kagera Sugar, George Kavila, alisema: “Ni mkongwe halafu ana uzoefu wa kutosha katika ligi yetu, najua uzoefu wake utamsaidia kwa namna moja ama nyingine kutusumbua, lakini naamini mbinu ambazo tumepewa na mwalimu wetu zitatusaidia kupata ushindi katika mechi hii muhimu.”