Mtibwa yaiingia anga za Yanga

Saturday January 13 2018

 

By DORIS MALIYAGA

Dar es Salaam. KIKOSI cha Mtibwa Sugar, kimewatambia Lipuli ya Iringa baada ya kuifunga nyumbani kwao bao 1-0,  na imepanda mpaka nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu.

Mtibwa iliyofunga bao hilo kupitia kwa Hassan Dilunga dakika 37 akiwatoka mabeki wa Lipuli, imefikisha pointi 24 na kuzipitia Yanga (21) na Singida United (23).

Akizungumzia mchezo huo mlinda mlango wa Mtibwa Sugar , Benedictor Tinocco amesema, wamecheza kwa kujituma ndiyo maana wameibuka na ushindi.

"Ilikuwa mechi ngumu lakini kujituma na kucheza kwa kufuata maelekezo ya mwalimu ndiyo maana tumefanikiwa,'anasema Tinocco.

Kwa upande wa Lipuli, Adam Salamba amesema, wamecheza vizuri lakini wapinzani wao walitumia nafasi wakawafunga.

Michezo mingine Ndanda FC imetoa sare ya 1-1 na Mbao FC  mchezo uliochezwa Nang'anda Sijaona wakati Stand United  imeifunga  Ruvu Shooting  bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

Katika michezo ya Ligi ya Daraja,  Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa Sh 2milioni kuwazawadia wachezaji wa Coastal Union baada ya kushinda 3-0 dhidi  Kurugenzi Mufindi.

Uamuzi huo wa Waziri ni kutimiza ahadi yake kwa timu hiyo ya Coastal Union ili kuhakikisha wanapanda kucheza Ligi Kuu msimu ujao. Mabao ya Coastal yalifungwa na Andrew Simchimba, Omary  Salum na Raizan Hafidi.

Matokeo ya michezo mingine, JKT Tanzania 3-0 Mvuvumwa, Kiluvya 1-3 Mgambo, Rhino 2-0 Dodoma, Mlale 1-0 Mawenzi, Biashara 2-0 Alliance, Toto 0-0 JKT Oljoro na Mshikamano 1-0 Ashanti United.