Msuva hakamatiki Ligi ya Mabingwa

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Taifa Stars, Saimon Msuva ameanza kufuata nyayo za Mbwana Samatta katika kufuamani nyavu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Samatta katika msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi cha TP Mazembe alifunga mabao sita katika Ligi ya Mabingwa rekodi ambayo inaweza kufikiwa na Msuva kama Difaa El Jadida itafuzu kwa hatua ya makundi.

Msuva alifunga bao lake la nne katika mashindano hayo akiwa akiingoza timu yake Difaa El Jadida kushinda bao 1-0 dhidi ya Vita Club, DR Congo katika mchezo wa awali wa hatua ya mtoano.

Akizungumzia bao hilo, Msuva amesema anajisikia furaha sehemu ya matokeo hayo licha ya wapinzani wao kucheza kwa kujilinda zaidi kwenye mchezo huo.

“Jamaa walikuwa wanacheza kwa kujilinda ili wasiruhusu bao, lakini uzuri tumepata ushindi, suala la idadi ya mabao ni muhimu ni bora kupata hata kidogo kuliko kukosa kabisa,” alisema mshambuliaji huyo.

Bao hilo alilofunga Msuva lilikuwa ni goli lake la manne ndani ya michezo mitatu ambayo amecheza mpaka sasa kwenye hatua hizi za mchujo.

Kabla ya mchezo wa marudiano ambao utachezwa Machi 18 nchini DR Congo, Msuva anategemewa kuingoza tena Difaa kwenye michezo miwili  ya Ligi Kuu Morocco dhidi ya FAR Rabat na Moghreb Tetouan.