Mshambuliaji wa Yanga hoi kwa Kijitonyama United

Muktasari:

Las Vegas ipo ligi daraja la pili ikisaka kupanda daraja msimu huu

Dar es Salaam. Mshambulaiji wa zamani wa klabu ya Yanga, Thomas Morris ameishudia timu yake ya Las Vegas ikichapwa mabao 3-0 na Kijitonyama United katika mchezo wa Ligi daraja la pili Kanda ya Dar es Salaam

Mchezo huo uliofanyika kwenye uwanja wa  Shule ya Msingi Mwananyamala B, ulikuwa mkali na wa kusisimua na Morris alichezea Las Vegas na kushindwa kuisaidia timu hiyo.

Kabla ya mchezo huo, baadhi ya wachezaji wa Las Vegas wakiongozwa na Morris walitamba kuifunga Kijitonyama United  si chini ya mabao5-0 katika mchezo huo wa kutafuta wawakilishi wa kanda ya Dar es Salaam katika ligi ya mabingwa wa mikoa.

Kijitonyama United iliyochini ya kocha, Saidi Seif na Ali Manywele iliwashtukiza Las Vegas kwa mpira wa kasi na pasi za uhakika na kupachikwa bao la kwanza kupitia kwa Sunday Timbuka kufuatia pasi safi ya Ali Babu.

Bao hilo lilimfanya Morris ambaye alikuwa kocha mchezaji, kuamua kuingia uwanjani  kwa lengo la kusawazisha na kusaka ushindi, hata hivyo hakufanikiwa kwani alikaribishwa na bao la pili lililofungwa na Ali Babu kufuatia ushirikiano mzuri na Ali Feruzi na Kulwa Ndege.

Pamoja na kujitahidi kusawazisha, Las Vegas walinyong’onyeshwa na bao safi la tatu lililofungwa na Ali Babu tena kufuatia pasi safi ya Abdallah Mnenga. Bao hilo lilishangiliwa na mashabiki wa Kijitonyama.