Mshahara wa Sanchez wamtoa udenda Pogba

Muktasari:

Ripoti zinadai Sanchez anaweza kutambulishwa kuwa mchezaji wa Man United rasmi leo Jumatatu, wakati Henrikh Mkhitaryan akitimkia huko Arsenal katika dili hilo.

MANCHESTER, ENGLAND. Mambo ni moto. Huko Old Trafford imeripotiwa Paul Pogba ameliamsha dude baada ya kutaka mshahara wake uongezwe mara mbili ili afikie ule atakaokuwa akilipwa Alexis Sanchez wa Pauni 450,000 kwa wiki.

Manchester United imempa ofa ya mkataba wa miaka minne na nusu mchezaji Sanchez, ambapo mshahara wake wa wiki utakuwa Pauni 350,000 pamoja na Pauni 100,000 za haki za taswira kwa wiki jambo linalomfanya kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi kwa wiki ndani ya Ligi Kuu England.

Lakini, kwa sasa wakala wa Pogba, Mino Raiola anajiandaa kuwaambia Man United mshahara wa Pauni 290,000 anaolipwa mteja wake kwa wiki hauendani na kiwango na hadhi ya mchezaji huyo.

Pogba ikifika mwishoni mwa msimu atakuwa amebakiza miaka mitatu katika mkataba wake aliosaini mwaka 2016 wakati aliponaswa na Man United akitokea Juventus kwa ada ya Pauni 89 milioni iliyoweka rekodi ya dunia kwa wakati huo.

Kwenye mkataba huo kuna kipengele ambacho Man United inaweza kumwongezea Pogba mwaka mmoja zaidi, kitu ambacho Raiola anataka kusimamia hapo kuhakikisha staa wake analipwa mshahara utakaomfanya alingane na Sanchez.

Raiola, anamsimamia pia Mkhitaryan pamoja na Romelu Lukaku, alitaka Mkhi alipwe fidia ya miaka yake miwili na nusu iliyobaki kwenye mkataba wake la sivyo angeweka ngumu kwa kuzuia dili hilo kufanikiwa.

Man United imeripotiwa kukubali. Huko Arsenal, Mkhitaryan atakuwa akilipwa mshahara wa Pauni 200,000 kwa wiki na kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi katika kikosi hicho cha Arsene Wenger.

Raiola siku zote amekuwa akihakikisha wateja wake wanabamba dili za pesa nyingi wanapopata dili la kujiunga na timu nyingine. Wakala huyo anamsimamia pia straika Zlatan Ibrahimovic.