Mourinho, Conte ni mshikemshike Old Trafford

Muktasari:

Timu hizo mbili zimekuwa na ushindani wa hali ya juu kila zinapokutana

MANCHESTER, ENGLAND. Kocha Jose Mourinho ameambiwa hivi ana matatizo matatu yanayokikabili kikosi chake wakati akielekea kwenye mechi dhidi ya Chelsea kesho Jumapili kwenye Uwanja Old Trafford.

Achana na ishu ya Paul Pogba, ambaye anaripotiwa kwamba ametibuana naye mazoezini na kumfanya Mourinho amtishie kiungo huyo kwamba yeye ndiye bosi klabuni Man United, hivyo anachopaswa kufanya ni kuafuata maelekezo yake anayotoa.

Wengine wanadai kwamba huenda Pogba akasugua tena benchi hiyo kesho kwenye mechi dhidi ya Chelsea ya Eden Hazard na Willian, aliyekuwa kwenye kiwango bora kabisa kwa sasa.

Shida tatu za Mourinho zinazoelezwa ni kwamba ni beki, Nemanja Matic na washambuliaji. Kukosekana kwa Eric Bailly kumeelezwa kwamba kumeifanya safu ya mabeki ya Man United kuonekana kuwa ya kawaida sana, jambo linalomfanya kipa David De Gea kuwa bize muda wote kuokoa michomo kutoka kwa wapinzani.

Chris Smalling, Phil Jones na Victor Lindelof hawaonekani kuwa na uwezo wa kumudu mashambulizi ya washambuliaji wakorofi kama hiyo kesho watakapokwenda kumkabili Hazard na Willian.

Hazard amekuwa na rekodi tamu dhidi ya Man United, ambapo katika mechi 14, ameshinda saba, sare tano na amepoteza mara mbili tu, huku yeye mwenyewe akipasia wavuni mara nne na kuasisti mara moja.

Hiyo ni rekodi inayoonyesha mabeki wa Man United watakuwa bize kweli kweli kumdhibiti staa huyo wa Ubelgiji. Shida ya pili ya Mourinho ni Matic.

Kiungo kwa sasa haonekani kama anaweza kunyonya mashambulizi ya upinzani wakati huo huo akiwa na kazi ya kupandisha mipira kushambulia kama anavyofanya N'Golo Kante huko Chelsea.

 Jambo hilo limemfanya Mourinho sasa kutafuta mchezaji mwingine wa kucheza na Matic na siku za karibuni amekuwa akimtumia Scott McTominay, baada ya kuona Matic anashindwa hata kuwalinda ipasavyo mabeki wao wa kati.

Shida ya tatu ipo kwenye ushambuliaji. Romelu Lukaku anaonekana kwamba bado hajazoeana vyema na Alexis Sanchez, huku ikielezwa pia Mourinho ameshindwa kumtumia staa wake mpya Sanchez ipasavyo na kumpa majukumu mengine uwanjani ambayo yanamzuia asitimize wajibu wake wa kufunga.

Kuhusu Lukaku, ni mshambuliaji anayehitaji mipira 10 kufunga mara moja, jambo hilo ndilo linalomfanya fowadi huyo kuwa na mabao 12 tu kwenye Ligi Kuu England hadi sasa wakati Harry Kane ameshatupia wavuni mara 23, Mohamed Salah mara 22 na Sergio Aguero mara 21.

Lukaku hapewi mipira ya kutosha, hivyo kuwa na wastani hafifu wa kufunga unaifanya Man United kutokuwa na uhakika wa kushinda, hasa zinapokuja mechi ngumu kama hizo dhidi ya Chelsea. Mourinho anavuka kizingiti hicho?

Mechi nyingine za Ligi Kuu England zitakazopigwa wikiendi hii, Leicester City watacheza na Stoke City huko King Power, wakati Bournemouth watamaliza ubishi na Newcastle United, Brighton watacheza na Swansea City, Burnley na Southampton, West Brom na Huddersfield, Watford na Everton, wakati Mohamed Salah na jezi lake la Liverpool watashuka Anfield kuwakaribisha West Ham United. Mechi nyingine ya kesho ukiachana Man United na Chgelsea ni Crystal Palace na Tottenham Hotspur.