Mfaransa Simba kila dakika 60 Sh42,000

Muktasari:

Lechantre ambaye kwa kila dakika moja ikiwa na maana sekunde 60 ya mshale wa saa inapogonga atakuwa akiingiza Sh700 katika mshahara wake usiopungua Sh30 milioni.

KOCHA Mkuu Mpya wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre anayetarajiwa kuanza rasmi kazi ya kuinoa timu hiyo kesho Jumanne na kumwezesha kuingiza kiasi cha Sh42,000 kwa kila dakika 60 yaani saa limoja amewapagawisha mastaa wa Simba.

Lechantre ambaye kwa kila dakika moja ikiwa na maana sekunde 60 ya mshale wa saa inapogonga atakuwa akiingiza Sh 700 katika mshahara wake usiopungua Sh 30 milioni amewaibua nyota wa zamani wa klabu hiyo waliomjadili kwa ujio wake.

Wengi wanatarajia makubwa kutoka kwake, lakini wakisisitiza ni lazima apate ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Wana Msimbazi ili kila kitu kiende sawa.

Straika wa zamani, Emmanuel Gabriel alisema kocha pekee hawezi kufanya timu ikafika kwenye mafanikio badala yake kila mtu awajibike kikamilifu na kwa nidhamu katika sekta yake.

"Nasisitiza kwamba wachezaji lazima wajue mipaka yao na wajue hawapo juu ya timu, lakini viongozi wahakikishe kila kitu kinafanywa kwa umoja asiwepo mtu ambaye anaona yeye bora kuliko mwingine, kila mtu akijiona ana wajibu na timu na ni sehemu ya timu Simba itakuwa ya kuotea mbali la, itakuwa cheza potea," alisema.

Naye Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema vipo vitu vingi ambavyo vinaweza kuleta mafanikio ndani ya klabu.

"Jambo la kwanza ni kumwacha kocha afanye majukumu yake kikamilifu, wachezaji wawe sawa asiwepo ambaye yupo juu ya mwingine, viongozi wawafanye watu wanaoipenda Simba kitu kimoja ndio maana nasema kocha pekee hawezi," alisema.

"Kikubwa ni kwamba viongozi wajaribu kuangalia makocha ambao wamewahi kupita ndani ya timu hiyo kisha wajue namna ya kusaidiana na huyu aliyepo," alisema Zamoyoni Mogella.