Mechi sita pointi nne, Yanga watafakari

Wachezaji wa Yanga.

Muktasari:

  • Hiyo inamaanisha nini? Jibu ni kwamba klabu zetu bado zina safari ndefu kwenye soka la Kimataifa na hiyo inamaanisha kwamba bado miundombinu yetu ni duni.

USHIRIKI wa Yanga kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho msimu huu umeibua mambo mengi. Ndiyo timu pekee ya Afrika Mashariki iliyoshiriki hatua hiyo baada ya klabu nyingine kushindwa kwa muda mrefu.

Hiyo inamaanisha nini? Jibu ni kwamba klabu zetu bado zina safari ndefu kwenye soka la Kimataifa na hiyo inamaanisha kwamba bado miundombinu yetu ni duni.

Katika hatua hiyo ya makundi Yanga imecheza mechi sita na kuambulia pointi tu ambazo ilizipata kwa ushindi dhidi ya MO Bejaia nyumbani na sare na Medeama. Matokeo hayo ya Yanga yanatoa picha halisi ya soka la Tanzania na Afrika Mashariki.

Tathmini ndogo ya soka la ukanda huu inaonyesha kwamba Yanga ndiyo klabu gumzo zaidi kwa sasa kutokana na usajili wake wa wachezaji ghali na mastaa wenye uzoefu kuliko klabu nyingine ambazo hazina misuli mikubwa kiuchumi.

Tajiri wa Yanga, Yusuf Manji amewawezesha kufanya usajili ambao umeitofautisha na klabu zingine za Kenya, Uganda, Rwanda na hata Tanzania kwenyewe. Katika Ligi za ndani imekuwa ikishinda inavyotaka lakini ushiriki wake kwenye michuano ya Shirikisho msimu huu umetoa picha halisi ya nini kilichopo katika soka yetu.

Yanga imeshindwa kuonyesha nguvu yake, tumeshuhudia katika mechi zote sita wachezaji walikuwa wakitumia nguvu akili na maarifa yao yote lakini maji yalizidi unga. Uwezo wao ulizidiwa maarifa na timu za nje, kupitia matokeo walionyeshwa kwamba bado wana safari ndefu na kwamba kipimo halisi cha ubora wao siyo ligi ya ndani.

Utofauti wake na klabu kama TP Mazembe, MO Bejaia na Medeama umeonekana kwenye mambo mengi. Kuanzia uchumi, maandalizi na mipango, aina ya wachezaji na umakini wao ndani na nje ya uwanja. Viongozi wao wanavyoyachukulia mashindano na jinsi wanavyojipanga na kucheza na timu pinzani kisaikolojia kabla na baada ya mchezo.

Ni mambo ambayo yalikuwa yanaipiga chenga Yanga kwa vile ilikuwa haijajipanga na muda mrefu ilikuwa haijashiriki hatua hiyo ya mashindano hivyo tunaamini kwa sasa kwamba imepata somo na imejifunza. Maoni yetu ni kwamba Yanga ijitafakari ilipotoka, ilipo na inapokwenda. Ifanye tathmini na tafakari ya kina ni nini kilichokea kule kwenye Ligi ya Mabingwa na huku kwenye Shirikisho na ijipange upya kwa kujirekebisha msimu ujao.

Uongozi, benchi la ufundi, wachezaji, wanachama na mashabiki wanapaswa

kujipima. Yanga inapaswa kuwa mtazamo mpya kwenye maandalizi na aina ya usajili inaofanya kwani umeonekana kupwaya. Kwavile bajeti ipo Kocha na benchi lake wanapaswa kufikiria zaidi ni aina gani ya wachezaji ambao wataisaidia Yanga kimataifa.

Uongozi unapaswa kuaanda bajeti ya maana ambao inawawezesha kwenda na mikikimikiki ya mashindano hayo. Lakini bajeti pekee haitakuwa na maana kama hakuna viongozi makini wanaoujua mpira ambao watasaidiana na benchi la ufundi kwenye mikakati.

Tumeona kabisa kwamba wenzetu wana Wakurugenzi wa ufundi na maafisa wenye uwezo mkubwa wa kiufundi wa kusoma timu pinzani na kutengeneza mfumo ambao utamrahisishia kazi kocha. Kuna wataalam ambao wanatumwa nje kwenda kusoma timu pinzani na wanakuja na siri ambazo zinamsaidia kocha kupata mwanga wa mechi ijayo, siyo lazima kila kitu afanye Kocha. Kama Yanga imeamua kuwekeza kwenye soka la kimataifa ijipange zaidi na kuongeza umakini kila hatua. Kwavile haitakuwa na maana kutumia nguvu kubwa na fedha nyingi kwa wachezaji ambao hawana uwezo wa kushindana kimataifa. Mafanikio siku zote huja kwa mipango madhubuti.