Mchawi wachezaji majeruhi Yanga atajwa

Muktasari:

Tangu kuanza msimu huu idadi kubwa ya wachezaji wa Yanga wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imeutaja Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuwa ndio chanzo cha mastaa wake kupata majeraha.

Tangu kuanza msimu huu idadi kubwa ya wachezaji wa Yanga wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Baadhi ya wachezaji majeruhi ni Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko, Andrew Vincent, Abdallah Shaibu na kinda Yohana Nkomola.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema Uwanja wa Uhuru ni chanzo cha nyota wake kuumia kwa kuwa sehemu ya kuchezea imeisha muda wake.

“Kusema kweli tuko katika wakati mgumu sana tangu msimu uanze, majeruhi wamekuwa wengi na kila siku wanaongezeka jambo ambalo linatuumiza kichwa,” alisema Mkwasa.

Kiungo huyo wa zamani wa Taifa Stars, alisema baada ya uchunguzi wa kina wamebaini uwanja huo ni chanzo cha matatizo.

Alisema Yanga wamekuwa wakitumia uwanja huo kwa mazoezi, hivyo wanatarajia kusaka mwingine ili kuepusha athari kubwa kwa wachezaji wake.

“Kapeti ya kuchezea (nyasi bandia) za Uwanja wa Uhuru imeisha muda wake inatakiwa kubadilishwa, wachezaji wanaumia mara kwa mara hata katika mechi tunazocheza tukimaliza lazima utasikia baadhi wamepata majeraha,”alisema Mkwasa.

Yanga inayonolewa na kocha Mzambia George Lwandamina, imekwenda Shelisheli na leo itaikabili St Louis katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Mechi ya kwanza Dar es Salaam ilishinda bao 1-0.