Mbaraka amerudi mzigoni

Muktasari:

Mbaraka alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, amerejea uwanjani na kama Kocha wake Aristica Cioaba akiamua kumpanga Jumamosi katika pambano lao dhidi ya Yanga, kazi itakuwapo Chamazi.

KAMA kuna jambo ambalo mashabiki wa Yanga hawapendi kulisikia ni hili. Mbaraka Yusuf, yule straika mwenye zali la kuwatungua Yanga anayekipiga na Azam kwa sasa, amerejea uwanjani wakati timu yake ikijiandaa kuikaribisha Yanga pale Chamazi.

Mbaraka alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, amerejea uwanjani na kama Kocha wake Aristica Cioaba akiamua kumpanga Jumamosi katika pambano lao dhidi ya Yanga, kazi itakuwapo Chamazi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mbaraka alisema anaendelea vizuri na yupo fiti kwa sasa na anatamani Kocha Cioaba amjumuishe katika kikosi cha timu yao dhidi ya Yanga.

Katika msimu uliopita Mbaraka akiichezea Kagera Sugar, aliwafunga Yanga magoli matatu katika mechi mbili za Ligi Kuu, mawili kwenye mechi iliyopigwa Kaitaba, Bukoba ambayo Yanga ilishinda 6-2 kisha kufunga jingine moja Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Nikicheza na timu kama Yanga na nikafunga ni kitu kikubwa na kitanirudisha mchezoni na kuendelea na kufunga kama ilivyo kawaida yangu. Lakini, kubwa ni kutaka kuona timu yetu inaondoka na pointi zote tatu uwanja wa nyumbani,” alisema.

Mpaka sasa Mbaraka ameifungia Azam mabao matatu na msimu uliopita akiwa Kagera alimaliza msimu akiwa na mabao 12 akifungana na Shiza Kichuya wa Simba na Obrey Chirwa wa Yanga.