Mayanja azipa mchongo Simba, Yanga kimataifa

KOCHA wa zamani wa Simba, Jackson Mayanja, amewaambia nyota wa kikosi hicho na kile cha Yanga wanapocheza michuano ya kimataifa waondokane na fikra potofu ya kwamba kuna baadhi ya timu hasa za mataifa ya Kiarabu hawawezi kutamba mbele yao.

Badala yake amewataka wacheze michuano hiyo kwa ari halisi ya kiushindani kwa lengo la kuwaondoa wapinzani wowote wanaokuja mbele yao, tofauti na vile ilivyozoeleka kuwa wao ni kuishia hatua za awali tu.

Baada ya kushinda mechi zao za kwanza nyumbani wikiendi iliyopita, wiki ijayo timu hizo zitakuwa ugenini kukamilisha raundi ya awali ili kujua kama zinasonga mbele ama la.

Yanga inayocheza Ligi ya Mabingwa Afrika na ambayo iliichapa St. Louis kutoka Shelisheli bao 1-0, itarudiana na wapinzani hao Jumatano ijayo siku moja baada ya Simba kufanya hivyo huko Djibouti mbele Gendermarie ambayo ililala 4-0 hapa nyumbani, mechi yao ni ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

“Ni wakati wa Simba na Yanga kuonyesha ukomavu wao. Zinatakiwa kuonyesha Tanzania inaweza kutwaa mataji katika michuano ya Afrika na si nchi ya kusindikiza wengine tu,” alisema Mayanja aliyewahi pia kuzinoa Kagera Sugar na Coastal Union.

Aliongeza kusema klabu hizo zina wachezaji wazoefu ambao wameshiriki mechi za aina hiyo mara nyingi na watakuwa wameshajifunza huwa wanakwama wapi.

“Unapozungumzia mechi za aina hii, hata Simba na Yanga ni wazoefu kama zilivyo klabu za Misri na kwingineko, cha muhimu wajue klabu wanazoshindana nazo zimewazidi wapi kisha wafanyie kazi madhaifu yao,” aliongeza.